Ruka hadi kwenye maudhui makuu

VIKOA VYA MAANA



VIKOA VYA MAANA
Dirk (2010), anasema kuwa vikoa vya maana ni jozi za maneno yenye maana zinazohusiana  ambazo maana zake zinategemeana na kwa pamoja zinatoa dhana ya kimuundo yenye uhalisia ndani yake. Hii humaanisha kwamba, maana ya haiponimu zinazotokana na kikoa kimoja hujumuishwa katika maana pana au jumuishi moja.
Wikipedia, wanaeleza kuwa kikoa cha maana ni msamiati wa kiufundi katika taaluma ya isimu ambao unaeleza kikundi cha maneno yanayohusiana kimaana.
Mahusiano ya maana katika vikoa vya maana huwa na sifa kuu mbili:
·         kila kikoa kinaweza kuzaa vikoa vingine vidogo vidogo. Kwa mfano; Matunda.
1.      Maembe,
2.      Machungwa, na
3.      Papai.
·         Hakuna kanuni ya upangaji wa hivyo vikoa. Kwa mfano; Matunda
1.      Papai
2.      Maembe, na
3.      Machungwa.
Hivyo kikoa cha maana kinaweza kufasiriwa kuwa ni mahusiano yanayotokana na seti yeyote ile ya msamiati na seti hiyo huwa katika kundi maalum la kimantiki. Baadhi ya mifano ya vikoa vya maana ni; “Uandishi wa kubuni” ambapo hujumuisha hadithi fupi, tamthiliya, ushairi na riwaya. “Michezo”; ambapo hujumuisha; mpira wa miguu, mpira wa kikapu, kuruka kamba, mpira wa pete, mpira wa meza na mpira wa mikono, na  “Nguo” ambapo hujumuisha suruali, shati, sketi, kanga, gauni, sidiria, na blauzi.

HAIPONIMIA/ HIPONIMIA
Briton (2000) anaeleza kuwa uhiponimia ni uhusiano wa kiwima ambapo hujumuishwa katika fahiwa na neno jingine. Kwa mfano fahiwa ya mgomba, mahindi na maharage zimejumuishwa katika mimea.
Matinde (2012) hiponimu ni neno ambalo lina maana mahususi amabayo hujumuishwa katika maana ya neno ambalo lina maana pana na uhiponimia ni uhusiano wa kifahiwa uliopo baina ya neno lenye maana mahususi na neno linguine lenye maana jumuishi.

Kwa mantiki hii tunabaini kuwa Tofauti kuu kati ya vikoa vya maana  na uhiponimia ni kwamba vikoa vya maana hujumuisha maneno yenye maana jumuishi wakati uhiponimia huwa na maneno yenye maana mahususi. Kwa mfano neno (mnyama) ni kikoa cha maana ambacho hujuisha simba, nyani, chui, nguruwe, pundamilia, tembo na kadhalika wakati neno (pundamilia) ni hiponimu amabayo huwa na maana mahususi yaani mnyama mwenye mistari myeupe na myeusi katika ngozi yake.



SIFA NA UMHIMU WA VIKOA VYA MAANA KATIKA MAWASILIANO
Kwa kuwa vikoa vya maana hujikita katika muktadha mmoja, huweza kuwa na sifazifuatazo katika mawasiliano;
Huonesha uhusiano wa maneno yenye sifa sawa au zinazoelekeana kimaana. Vikoa vya maana humsaidia mwanaisimu kutambua sifa za maana mbalimbali zinazohusiana kimaana. Hii humaanisha kuwa, huwezi kuweka neno fulani katika kikoa fulani bila kujua sifa zinazotawala neno hilo. Hivyo basi, haiponimu zote zinazotokana na neno moja pana huwa na sifa ama zinazofanana au zinazo elekeana. Kwa mfano, lazima ujue neno matunda lina sifa zipi ndipoutaweza kutaja au kuorodhesha matunda yanayojenga kikoa hicho kama vile ndizi, embe, nanasi,chungwa, na papai.

Hurahisisha mchakato wa ujifunzaji lugha. Vikoa vya maana husaidia kumuelekeza mtu anayejifunza lugha fulani mahususi ili kujua vitu mbalimbali vilivyowekwa katika kundi Fulani husika. Kwa mfano, mtu mgeni wa lugha fulani huweza kujifunza kuwa, dhana ya neno “matunda”, hurejelea ndizi, maembe, parachichi, zabibu na machungwa. Kwa mantiki hii, mgeni wa lugha fulani anapotajiwa moja ya vitu vilivyoorodheshwa hapo juu, mfano ndizi, maembe au zabibu, ataelewa kuwa kinacho maanishwa au kinacho rejelewa ni matunda.

Hurahisisha mawasiliano. Katika mawasiliano, matumizi ya neno moja pana linalo rejelea maana nyingine ndogondogo husaidia kuokoa muda baina ya wazungumzaji. Kwa mfano, mtu anapokwenda sokoni, badala ya kutaja kitu kimoja kimoja, huweza kutaja kwa ujumla wake endapo vinahusiana. Mtu akienda sokoni huweza kuuliza; “una mboga za majani?”. Atajibiwa; “kuna mchicha, chainizi, spinachi, na matembele”.

Vikoa vya maana husaidia katika shughuli za utunzi wa leksikografia. Mdee (2010),akimnukuu Wiegand, anaeleza kuwa, leksikografia ni kazi ya kisanaa inayojishughulisha na utunzi wa kamusi. Leksikografia hiyo hujishughulisha na ukusanyaji wa misamiati mbalimbali yalugha na ndiyo inayosaidia kutungiwa kamusi. Kamusi ni kipengele cha kisemantiki kwa kuwa hutoa maneno yenye maana kwa watumiaji wa lugha. Maneno hayo huweza kutumika kamavikoa vya maneno vyenye maana. Mifano ya kamusi zenye vikoa vya maana ni kama vile;
·                  kamusi ya wanyama 
·                  Kamusi ya mavazi 
·                  Kamusi ya tiba ya magonjwa 
·                  Kamusi za misuko ya nywele 
·         Kamusi za vyakula

Kikoa kimoja huweza kusaidia kujua na kufafanua vikoa vidogovidogo vilivyomo ndani ya kikoa kikubwa. Kwa mfano, mtu anapokwenda hotelini na kusema; “naomba chakula”,ataulizwa, “unahitaji ugali, ndizi, viazi, au wali?”. Kisemantiki, hii humsaidia mtumiaji wa lugha kuteua kikoa mahususi kwa ajili ya matumizi yake kwa wakati huo. Kwa mfano, mtu atasema; “nahitaji ndizi”.

Husaidia kuonesha umbo la wingi ambalo lina umuhimu kisemantiki hasa katikaupatanisho wa kisarufi. Kwa mfano, badala ya mtu kusema, “kikoa cha mmea” husema “kikoa cha mimea”, badala ya kusema “kikoa cha ua” atasema “kikoa cha maua”. Vikoa hivyovinapotumika kwenye sentensi huwa “mimea imeota” badala ya kusema “mmea imeota”, “Ualimechanuza”  badala ya kusema “maua limechanuza”.

Vikoa vya maana vina sifa ya kuwa na maana ya kileksimu na kufanya kikoa kimoja kichanuze zaidi na kuweza kupata maneno mengine yenye maana kisemantiki. Kwa mfano, kunakikoa cha masomo ya sayansi, baiolojia, fizikia, kemia na kilimo. Kikoa cha baiolojia kinaweza kufasiliwa kuwa ni somo la kisayansi linalohusiana na viumbe hai na visivyo hai. Hivyo tunaona kuwa kikoa cha baiolojia kimechanuza zaidi na kuleta maana ya kikoa hicho.

MAREJEO
Brinton L. J. (2000). The Structure of Modern English. A Linguistic intro Illustrated edition. John Benjamini Publishing company.

Dirk, G. (2010). Theories of Lexico Semantics. Oxford university Press: New York.
 
Mdee, J. S. (2010). Nadharia na Historia ya Leksikografia. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili: UDSM

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

UCHAMBUZI WA RIWAYA ZA “NAGONA” NA “MZINGILE”

UCHAMBUZI WA RIWAYA ZA “NAGONA” NA “MZINGILE” 1.0 Utangulizi Katika makala haya tutachambua riwaya za ‘Nagona’ na ‘Mzingile’. Katika kuchambua riwaya hizi tutajikita katika kuangalia baadhi ya vipengele kama dhamira, falsafa, lugha, mtindo wa usimulizi, wahusika, motifu na suala la ontolojia. 2.0 Maelezo kuhusu mwandishi na riwaya zake 2.1 Maelezo kuhusu mwandishi Euphrase Kezilahabi alizaliwa mwaka 1944 katika kijiji cha Namagondo kilichoko kisiwani Ukerewe katika ziwa Victoria nchini Tanzania. Alipata elimu ya msingi huko kijijini Ukerewe na baadaye alijiunga na seminari ndogo ya Nyegezi kwa ajili ya masomo ya upili. Baada ya kumaliza alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es salaam mnamo mwaka 1967. Katika masomo yake alijishughulisha na nadharia mbalimbali zihusuzo falsafa (Wamitila 1991:64). Mnamo mwaka 1976 alitunukiwa shahada ya umahiri ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, kabla ya kutunukiwa shahada nyingine ya umahiri ya Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison mwaka 1982. Mwaka...

UCHAMBUZI WA FANI NA MAUDHUI KATIKA RIWAYA YA “ADILI NA NDUGUZE” ILIYOANDIKWA NA SHAABAN ROBERT

  1.0   Utangulizi Kazi hii inahusu uchambuzi wa fani na maudhui katika riwaya ya “Adili na Nduguze ” iliyoandikwa na Shaban Robert mwaka 1952. Katika kujadili riwaya hii tutaeleza dhana ya riwaya, usuli wa mwandishi, muhtasari wa kitabu chenyewe, nadharia zitakazotumika kuchambua fani na maudhui ya kitabu hiki, uchambuzi wa fani na maudhui na hitimisho. 1.1 Dhana ya Riwaya Kwa mujibu wa Madumulla (2009) akimrejelea Msokile (1992) anafafanua kuwa riwaya ni kazi ya sanaa ya kubuni, ni maandishi ya nathari (ujazo) yanayosimulia hadithi ambayo kwa kawaida ina uzito, upana, urefu wa kutosha, ina wahusika wengi wenye tabia mbalimbali, ina migogoro mingi mikubwa na midogo. Senkoro (1982) anasema riwaya ni hadithi ndefu ya kubuni yenye visa vingi, wahusika zaidi ya mmoja, na yenye mazungumzo na maelezo yanayozingatia kwa undani na upana maisha ya jamii. Wamitila (2003), Samwel na wenzake (2013), wanasema kuwa riwaya ni kazi andishi ya fasihi ambayo...