UCHAMBUZI WA RIWAYA YA WALENISI
JINA
LA KITABU: WALENISI
MWANDISHI: KATAMA MKANGI
MWAKA: 1995
MCHAPISHAJI: East African
Educational Publishers Ltd.
HISTORIA
YA MWANDISHI
Katama Mkangi
ni profesa wa
taaluma ya elimu-jamii. Hata hivyo
ni msomi ambaye
amebobea katika Nyanja
mbalimbali zikiwemo lugha
na fasihi ya
Kiswahili. Mkangi ni mwalimu, mhadhiri na
msomi ambaye amejishughulisha na
masuala ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na
kiutawala; sio tu
katika maandishi bali katika
harakati zake za
maisha ya kila
siku.
Itakumbukwa kuwa
katika uchaguzi mkuu
wa mwaka 1997
aligombea kiti cha
urais wa Jamhuri ya
Kenya, lakini hakufaulu. Kwa
sasa yeye ni mhadhiri
wa taaluma ya
kijamii katika chuo
kikuu cha USIU-Africa. (United State
International University of
Africa-Kenya).
Pamoja na
Walenisi, riwaya zake nyingine
ni Ukiwa na
Mafuta. Riwaya ya Walenisi
inaakisi masuala kemkem
yanayoiathiri jamii kama
vile ukandamizaji, matumizi mabaya
ya sheria, kutokuwa na
usawa, utawala mbaya, ulevi, na
mambo mengine mengine.
USULI
/MUHTASARI WA RIWAYA
Walenisi ni
riwaya ya kisira (kiwasifu) inayomsawiri
mhusika Dzombo katika
siku zake za
hukumu. Dzombo anahukumiwa kifo
kwa hatia bandia. Anang’oa nanga ya
sayari, chombo kinachopaswa kumwangamiza
na hatimaye chombo
hicho kinamwepusha na
hukumu hiyo na
kumpeleka ulimwengu tofauti
na atokao.
Aliowakuta huko
sio wengine bali
ni Wawalenisi ambao
Dzombo kutokana na
wanavyoishi alidhani yuko
peponi (mbinguni) kumbe sio.
Alijifunza mambo mengi
kuhusu sababu ya Wawalenisi kuishi
maisha mazuri, kupendana,
kushirikiana, na kuwajibika ikiwa ni
baada ya kuwaondoa
wachuna siku ya
mapambazuko na hatimaye
wakajikomboa na unyonyaji
na unyanyasaji wa
wachuna uliokuwepo awali.
Hatimaye Dzombo
anaamua kurudi duniani (jehanamu) ili kuwaamsha
watu waweze kujenga
jamii mpya au
ulimwengu mpya usio
na karaha.
NADHARIA ZILIZOTUMIKA
Nadharia
ya fasihi ni chombo
cha mawazo kinachotumika
katika usomaji wa
fasihi kwa vitendo. Katika riwaya
ya Walenisi mwandishi
ametumia nadharia zaidi ya moja
kuiumba kazi yake.
(1) Nadhaaria ya
Uhalisia.
Ni nadharia
inayoelezea ukweli wa
mambo katika jamii
na kusuta maovu
yaliyomo katka jamii. Katika
riwaya Walenisi nadharia
hii imejidhihirisha kwa
kuonesha maovu kama vile
unyonyaji, matabaka, dhuluma, unyanyasaji na
mengineyo.
(2) Nadharia ya
mwingiliano matini.
Ni nadharia
au dhana inayoongelea
uhusiano wowote unaoweza
kuonekana katika matini
moja na nyingine. Katika riwaya
hii msanii ameweza
kutumia matini mbali mbali
akiwa amekusudia kufikisha
ujumbe wake ipasavyo. Mfano: Ameweza kutumia
nyimbo katika ukurasa
wa 111 hadi
113 na pia
ukurasa wa 214. Vilevile ametumia sala (uk.147).
“Baba yetu uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe. Ufalme wako na uje. Mapenzi yako
yatendeke hapa duniani kama
yatendekavyo huko mbinguni…”
Vilevile ametumia
matini ya ushairi
kwa lengo lile
lile la kufikisha
ujumbe aliokusudia. Mfano:
ukurasa wa 197.Pia matini
nyingine ni ya
majibizano baina ya
mhusika mmoja na
mwingine (daiolojia).
(3) Nadharia ya
U-Maksi.
Ni nadharia
ambayo wazo lake
kuu ni kuwa
harakati za matabaka
ndio msingi mkuu
unaofanya mambo yawe kama
yalivyo duniani. Nadharia
hii husisitiza juu
ya uyakinifu wa
maisha, harakati za kitabaka, kupinga unyonyaji
na kudadisi, kupinga na
kulaumu hali zote
zilizoanzishwa na mabwanyenye.
Katika riwaya hii
ya Walenisi u-maksi
unajidhihirisha kwa kupinga
unyonyaji (uk.155-165), matabaka
(uk.80,85,71, 168-169), na
kusisitiza uzalishaji mali
na uwajibikaji kwa wote. Mfano (uk.111-115) na
(uk.108-109).
UCHAMBUZI WA
FANI NA MAUDHUI
A: MAUDHUI
Maudhui ni
jumla ya mawazo
yote ya mwandishi
aliyokusudia kuyafikisha kwa
jamii husika. Maudhui
hujumuisha vipengele mbalimbali
kama vile;
DHAMIRA
Haya ni
makusudio au malengo
ya mwandishi kwa
jamii husika. Katika
kipengele hiki zipo
dhamira kuu na
dhamira ndogondogo.
Dhamira kuu
Ujenzi wa
jamii mpya/ulimwengu mpya
usio na karaha.
Mwandishi wa
riwaya hii Katama
Mkangi analielezea suala
hili kwa kutumia
mhusika Dzombo kama
mwanamapinduzi anayetaka kujenga
jamii mpya, jamii ambayo
haina mambo maovu
kama vile unyonyaji, dhuluma, matabaka, unyonyaji na
mengine mengi kama
hayo. Anataka kuwe
na jamii kama
ya Wawalenisi waliokuwa
wakiishi maisha mazuri
ya ushirikiano, usawa, uhuru,
amani na
upendo. Mwandishi anaeleza
kuwa kuumizana, katu kuoneana, katu kupapurana, katu kuzomeana, katu kunyanyasana, katu kuibiana,n.k (uk.79).
Mwandishi anaeleza
kuwa kabla ya Walenisi
kulikuwepo jamii ya
wachuna ambayo ilijigawa
katika matabaka, yaani tabaka
la wachuna (matajiri) na tabaka
la masikini walionyanyaswa. Hatimaye
tunamwona mhusika Dzombo
baada ya kujionea
hali halisi ya
maisha waliyoishi Wawalenisi
anaamua kurudi duniani (Jehanamu) ili
akawaamshe ndugu na
jamaa zake wanaoteseka.(uk.194)
Dhamira ndogondogo.
(i)
Matabaka
Hii
ni hali ya
kuwepo kwa makundi
mawili tofauti ya
kijamii. Makundi haya
yaweza kuwa ya
wenye navyo na
wasio navyo au
wenye upeo na
wasio na upeo.
Mwandishi analielezea suala
hili kwa kutumia
Walenisi walivyokuwa wakiishi
enzi za wachuna.
“Wachuna walijitenga na
kujigawa kimaisha. Kwao
maskani walikokuwa wakiishi
kukaitwa mijini na
kwa wengine mashambani.
Jamii ikawa imejigawa
katika vipande viwili, mjini
na shamba, tabaka la
mla na mliwa, daraja
mbili akili na
tani. Pia tabaka
la tajiri na masikini”.(uk.168-169),
vilevile (uk.71, 80 na 85).
(ii) Umasikini
Umasikini ni
hali ya mtu
kutoweza kujikimu kimaisha.
Katika riwaya hii
mwandishi amelielezea suala
hili kwa mapana
huku akimtumia mhusika
Dzombo na Masikini
Jeuri katika maisha ambayo waliishi.
“Paa lilijaa mianya, kuta
za udongo zilikuwa
na viraka vya
kanja, makuti mabovu na
makaratasi ya makatoni.
Walipokuwa wamekaa ndipo
palikuwa pa kulala, kupikia, kuzungumzia na
pa kila kitu
ambacho nyumba zapaswa
kusitiri”. (uk.72-74).
Vilevile hali hii
inajidhihirisha (uk.126-127) na
pia (uk.114) ambapo
anasema kuwa, kuomba omba
ndiyo yalikuwa maisha
yao, na mwisho
kifo kikawa mkombozi
wao.
(iii) Unyonyaji
na unyanyasaji
Ni kutokuwepo
usawa baina ya mtu na mtu
au kundi moja la watu dhidi ya jingine , hali ambayo
husababisha matabaka. Mwandishi
amejadili suala la
unyonyaji na unyanyasaji
kwa kutumia watu
wa jamii ya
wachuna. Wachuna walikuwa
wakiwanyanyasa wenzao ilihali
wao wakiishii maisha
mazuri. Baadhi yao
walitokea katika jamii ya
mabavu, moto, wachawi, ambao
walitumia sheria na
mabavu kuwakandamiza wenzao. (uk.155-165).
Hali ile ile
ilitokea kwa Dzombo
na ndugu yake, hasa
anapomwambia ndugu yake
kuwa hali ya
ufukara wao ilitokana
na kunyanyaswa na
tajiri wao. Kwa
kuwa ndugu yake
hakujua maana ya
kunyonywa, kesho yake ali
mwendea tajiri wao
na kumwambia, “Hebu name
nikunyonye”.(uk.14-15).
(iv) Uwajibikaji
Mwandishi Katama
Mkangi amelionesha suala
hili kwa kutumia
au kurejelea jamii
ya Walenisi. Amewagawa
katika marika manne
ambayo yalijulikana kama
Rika Dunge (Watoto), Rika Hirimu
(vijana chipukizi), Rika Kambi
(makamu) na Rika Vaya
(wazee). Kila rika
lilikuwa na wajibu
wake katika jamii
au jukumu la
kitaifa. Jinsia zote
zilijihusisha katika majukumu
yote ya kitaifa,
si wanawake, si wanamme,
si wasichana si
wavulana. “Kumbo ambalo
halikutimiza wajibu wake, ama
rika moja kupuuza
wajibu wake, basi lilichukuliwa
kuwa limezorotesha taifa
zima na baadaye
kuoneshwa kwa kinamna
gani limefanya hivyo”.(uk.108-109) vile
vile (uk.111-115).
(v)
Rushwa na ufisadi
Rushwa ni fedha au kitu cha thamani, kinachotolewa
na kupewa mtu mwenye mamlaka ya jambo Fulani ili mtoaji apatiwe upendeleo.
Ufisadi ni hali
ya kuhujumu mali
ya wengi kwa
minajili ya kujinufaisha
mtu binafsi. Mwandishi anajadili
suala la
rushwa katika riwaya
yake kwa kumtumia
mhusika Mzee Matingasi
ambaye hakuwa na
leseni na alikuwa akitoa rushwa
kwa maaskari ili
asizuiwe kufanya biashara
zake. Aliweza kuhepa
vikwazo vya sheria
kwa ukarimu wake
kwa kumpa chupa
mbili au tatu
ama pesa taslimu
kwa askari aliyejaribu
kumzuia. (uk.91). Pia mwandishi
ameonesha suala la
ufisadi katika jamii
ambapo watu wachache
hujirundikia mali ama
utajiri kwa kibinafsi
na kufanya kuwa
urithi wao. Mfano:(uk.83_85).
(vi) Nafasi
ya mwanamke
Katika riwaya
ya Walenisi, mwandishi Katama
Mkangi amemchora mwanamke
katika nafasi mbalimbali kama
ifuatavyo:-
·
Mwanamke kama
kiongozi.
Mwanamke amechorwa kama mtu anayeweza
kusimamia au kuongoza
shughuli fulani (madaraka
fulani). Mfano: Mtu-Binti Fikirini
aliyekuwa Mkurugenzi mkuu
wa kiwanda cha
kutengeneza Trimi. (uk.97).
·
Mwanamke kama
mtu wa kudharauliwa
na kutothaminiwa katika
jamii.
Mfano mzuri ni
kijijini kwa Dzombo, hasa
pale mlevi mmoja alipowatukana
wanawake kwa kusema
wote ni Malaya, anaendelea kusema, “mimi si mototo
wa mwanamke…mimi ni mototo wa
mwanamme”.(uk.92). Mwandishi anapiga
vita kauli ya namna hii
kwa kumtumia mwanamke
aliyesema, “Ni nani aliyekwambia
kuwa huyo umuitaye
baba yako ndiye
baba yako?”… “Unamwaminije mamako?”
(uk.93).
·
Mwanake kama
mtu mwenye hekima. Mfano
mzuri ni katika
ukurasa wa 123
mwandishi anapoandika,
“Mwanamke amekuwa kitovu
cha hekima kwa
sisi Wawalenisi, hatukomi kufurahia
ukweli huu”.
·
Mwanamke kama
mlezi wa familia. Hali
hii inajidhihirisha kwa
mhusika Mama-mtu Maanani
aliyeilea na kuitunza
familia yake na mgeni wao
Dzombo. Vile vile
mhusika Hani(Mama Chizi)
ambaye ni mke
wake Dzombo aliwalea
watoto wake, ukiachilia mbali
umasikini waliokuwa nao.(uk.126).
MOTIFU
Motifu ni
matukio yanayojirudia rudia
katika kazi ya
fasihi, kuanzia mwanzo hadi
mwisho wa kazi
hiyo. Katika riwaya
hii ya Walenisi
kuna motifu tofauti
zilizojitokeza.
(i)Motifu
ya safari. Motifu
hii imeonekana kwa
kiasi kikubwa kuanzia
sura ya kwanza
tunapomuona Dzombo
akipewa sayari kama
chombo cha kwenda
kumuangamiza, lakini
anakitumia vizuri na
kukiendesha hadi kinapompeleka
katika ulimwengu mwingine.
Lakini pia anapofika
huko motifu hii
inaendelea anapoanza kusafiri
kwa Trimi sehemu
mbali mbali, na baadaye anaposafiri
kurudi kwao (Duniani au
Jehanamu).
(ii)Motifu
ya mapambano. Motifu
hii pia imejidhihirisha katika
riwaya hii, hasa tunapomuona
mhusika Dzombo akipambana
na unyonyaji na unyanyasaji
katika jamii yake
na baadaye majabali
mbalimbali akiwa kwenye
sayari na kuyashinda.
Lakini pia anapoamua
kurudi duniani (Jehanamu) kupambana
na hali iliyokuwepo
ya unyonyaji na
unyanyasaji wa watu wachache.
(iii)Motifu ya
ukombozi.
Hii pia ni motifu nyingine
inayoonekana katika riwaya
ya Walenisi. Motifu
hii pia inamhusu
mhusika Dzombo aliyefanya
harakati kwa lengo
la kujikomboa toka
kwenye sayari aliyokuwemo, lakini pia
kuikomboa jamii yake
iliyotawaliwa na unyonyaji na
dhuruma nyingi. Vilevile
katika nchi ya
walenisi tunaambiwa kuwa
hapo awali walitawaliwa
na tabaka la
wachuna lakini baadaye
wakajikomboa toka mikononi
mwao.
ONTOLOJIA
Ontolojia ni jambo ambalo jamii
fulani huliamini sana na kulishikilia
kwa wakati husika.
Katika riwaya hii
kuna ontolojia kadhaa
zilizoonekena.
(i)
Imani
kuwa mwanamke hawezi
kuwa kiongozi katika
ngazi fulani. Mfano
mzuri ni kwa
Mtu-Binti fikirini akiwa
kama mkurugenzi mkuu
wa kiwanda cha
Trimi, Dzombo alishangaa hali
ile ya mwanamke
kuwa na wadhifa
mkubwa kama ule, kitu
ambacho kwao hakikuzoeleka. (uk.97).
(ii)
Pombe
kama suluhisho la
matatizo. Ontolojia hii
inawakuta jamii ya Dzombo
ambao waliamini kuwa
suluhisho la matatizo
ni kunywa pombe.
Mfano ni Dzombo
na mwenzake Maskini
Jeuri walipoamua kwenda
kunywa pombe baada
ya kukosa mafuta
ya taa na
kibatari kulipuka. (uk.74-75).
(iii)
Mwanamme
kutoa mahari anapotaka
kuoa. Hali hii
pia inajikita katika
jamii ya akina
Dzombo ambao kwao
huu ulikuwa utamaduni
wao kama ilivyo
kwa jamii nyingi
za kiafrika. Lakini
alipokuwa katika ulimwengu
wa Walenisi, Mtu-Binti fikirini
alimwambia kuwa, wao
hawaoani kwa mahari; hawauzani wala
kununuana. (uk.134).
(iv)
Imani
kuwa Mungu ndiye
mwenye mapenzi ya
kweli. (uk.147).
(v)
Imani
kuwa watu wenye
ngozi nyeupe ndio
wenye akili, ili-hali wengine
ni kama wanyama. (uk.143).
UJUMBE
Funzo
tunalopata baada ya
kusoma kazi ya
fasihi. Katika riwaya
ya Walenisi tunaweza kuona
jumbe mbalimbali kama ifuatavyo:-
- Rushwa
ni adui wa
haki katika jamii.
- Kidole
kimoja hakivunji chawa.
- Umoja
na mshikamano ni
chachu ya maendeleo
katika jamii.
- Elimu
ni kitu muhumu sana
kwa kila mwanadamu.
-
Kufanya kazi kwa
bidii ni chachu
ya maendeleo katika
jamii.
- Mwanamke
sio mtu wa
kudharauliwa kama wengi
wanavyoamini.
MIGOGORO
Ni hali
ya msuguano au
kutoelewana baina ya pande mbili.
Kutoelewana huko kwaweza
kuwa baina ya
mtu na mtu,
kundi la watu dhidi ya lingine,
mtu na kundi
la watu, n.k.
Katika riwaya hii
migogoro imejitokeza katika mwonekano tofauti
kama ifuatavyo.
(a) Mgogoro kati
ya Dzombo na tabaka tawala.
Chanzo chake ni
kitendo cha Dzombo
kudai haki yake
na suluhisho lake
ilikuwa ni kuhukumiwa
kifo.(uk.1).
(b) Mgogoro kati
ya Dzombo na
tajiri. Chanzo chake
ilikuwa ni unyonyaji
wa tajiri, suluhisho
lake ni Dzombo kufukuzwa
kazi.(uk.14 na 15).
(c) Mgogoro kati
ya Dzombo na karani. Chanzo cha
mgogoro huu ni
kitendo cha Dzombo
kupanda mahindi ambayo
hayakutakiwa na tabaka
tawala. Suluhisho lake
likawa ni tabaka
tawala kufyeka mahindi
ya Dzombo na kuamuru
alime mazao waliyoyataka
wao.(uk.19 na 20).
(d) Mgogoro kati
ya tabaka la juu na
tabaka la chini katika jamii ya Wachuna. Chanzo
chake ni unyonyaji
na unyanyasaji, Suluhisho lake
ni mapinduzi ya kiutawala.
(e) Mgogoro kati ya mlevi
na mwanamke. Chanzo
chake ni mlevi
kuwadhalilisha wanawake kuwa
wote ni Malaya, Suluhisho lake
ni kueleweshwa kuwa
hata yeye ni
mwana wa mwanamke.(uk.92-94).
FALSAFA YA
MWANDISHI
Mwandishi Katama
Mkangi anaamini kuwa
ukweli ukijidhirisha basi
uongo hauna budi
kujitenga. Pia anaamini
kuwa sauti ya wengi ndiyo sauti
ya Mungu.(uk.195) Mwandishi
pia anaamini kuwa
endapo ulimwengu mpya
utakombolewa, basi binadamu ataishi
duniani kama peponi
(mbinguni).
MSIMAMO
Msimamo wa
mwandishi ni upande
anauegemea anapotunga kazi
ya fasihi. Msimamo
wa Katama Mkangi
ni wa kimapinduzi, kwani anaeleza
maisha ya Walenisi
walivyoishi maisha mazuri
katika ulimwengu mpya
na huru usio
na karaha baada
ya kuwaondoa wachuna
(wanyonyaji, wakandamizaji, wadhalimu, wauaji ). Pia
Dzombo anapoamua kurudi
duniani (Jehanamu) kuwaamsha
wenzake, mwandishi anakiita kitendo
hiki ni uwalenisi
halisi na ushindi. (uk.217).
MTAZAMO
Katika riwaya
hii ya Walenisi
mtazamo alioutumia mwandishi
ni wa kiyakinifu.
Yeye anaamini kuwa
ulimwengu utabadilika endapo
watu wa chini
wataamua kuungana pamoja
na kupambana na
tabaka linalowakandamiza. Mwandishi
anaonesha jinsi watu
walivyomulikwa na nuru
za ufahamu, hatimaye wakaamuka
na kuuamsha ulimwengu
wote na mwishowe
kuwapindua wachuna na
hatimaye jamii ya
Walenisi kutokea.
B:
UCHAMBUZI WA FANI
Fani ni
ufundi au ujuzi
anaoutumia msanii au
mwandishi katika kuumba
kazi yake ya
kifasihi. Katika kipengele
hiki cha
fani kineundwa na
vipengele mbalimbali kama
ifuatavyo:-
MUUNDO
Ni mpangilio
wa visa na
matukio katika kazi
ya fasihi. Muundo
upo wa moja
kwa moja, rejea na Rukia.
Mwandishi
ametumia muundo wa
Rejea kwa kuyapanga
matukio katika sura
tisa. Sura ya
kwanza tunamwona mhusika
mkuu Dzombo anahukumiwa
kifo, lakini hatujaona
sababu ya kuhukumiwa
kwake. Chombo kinachotakiwa
kumwangamiza ni sayari, lakini anakiongoza
vizuri na kujiepusha
kifo na hatimaye
kinampeleka ulimwengu mwingine.
Tunapata sababu ya
kuhukumiwa kwake katika
sura ya 2
na ya 4.
Mwishoni Dzombo anaamua
kurejea duniani (Jehanamu).
MTINDO
Ni jinsi
au namna mwandishi
anavyoiunda kazi yake
kuitofautisha na kazi za wasanii
wengine. Katika riwaya
ya Walenisi mwandishi
ametumia mtindo wa
masimulizi (monolojia) na
kwa kiasi kidogo
mtindo wa majibizano
(daiolojia) kati ya
wahusika.
Mwandishi ametumia
nafsi ya tatu (III)
na kwa kiasi
kidogo nafsi ya
kwanza na ya
pili (I na II). Mfano (uk.16,19,126
na 127). Vile
vile mwandishi ametumia
vipengele vya fasihi
simulizi kama vile
misemo, methali na nyimbo. Mfano; Wimbo
umeonekana (uk.111 hadi 113
na214). Shairi pia
limeonekana (uk.197).
WAHUSIKA
Ni watu
au wanyama wanaotumiwa
na mwandishi katika
kazi ya fasihi
kwa lengo la
kufikisha ujumbe aliokusudia
kwa hadhira. Katika
kipengele hiki kuna
wahusika wakuu na
wahusika wasaidizi au
wadogo.
(a)
WAHUSIKA/MHUSIKA MKUU
DZOMBO
·
Ni
mhusika mkuu (bapa) kwani hakubadilika
kitabia na kiimani
toka mwanzo hadi
mwisho wa riwaya.
·
Ni
mwanamapinduzi.
·
Ni
mchapa kazi/mwajibikaji.
·
Ni
mzazi na mlezi wa
familia ya watoto
watano.
(a)
WAHUSIKA WADOGO/WASAIDIZI
·
Mtu
Binti Fikirini
-Alikuwa mkurugenzi
mkuu wa kiwanda
cha Trimi (uk.97).
-Aliolewa na
Dzombo (uk.216).
-Alikuwa mrembo
(uk.62)
·
Mama
Mtu Maanani
-Alikuwa mlezi
wa familia.
-Alikuwa mama
mwenye huruma na
busara.
-Alikuwa mume wa mtu-mzee mwenzio
·
Mama
Mtu Pendo
-Ni mlezi
na mwenye mapenzi
bora kwa watoto.
-Anaamini kuwa
mkataa mtoto basi
ni mchawi.
·
Mtu
Binti Hekima
-Ni binti
mwenye hekima na
busara nyingi.
-Alimshauri dada
yake (Mtu Binti
Fikrini) juu ya
uhusiano wake na Dzombo.
·
Mzee
Mtu Mwenzio
-Ni baba
wa familia ya
watoto sita na
mke mmoja.
-Ni mzee
mwenye huruma na
busara
·
Mtu
Nasi. Alikuwa mwanasayansi.
·
Mtu
Makazi. Alikuwa katibu
wa kiwanda cha
Trimi.
·
Mtu
Wazo, Mtu Tabia, Mama
mtu Pendo.
·
Masikini
Jeuri. Ni mtu
masikini sana lakini
haoni kama umasikini
wake unampunguzia chochote.
Anaamini kuwa suluhisho
la mawazo kwa
mtu ni kunywa
pombe.
·
Hani (Mama Chizi).
Ni mke wa
Dzombo. Ni mlezi
wa familia ya
watoto watano. Ni mvumilivu,
hasa baada ya
hukumu ya mme
wake aliendelea kuwalea
watoto wake.
·
Chizi, Umazi, Tsuma, Munga na
Chai. Ni watoto
wa Dzombo.
·
Mabavu.
Ni mhusika shujaa
mwindaji. Ni mwanzilishi
wa sheria.
·
Kadzo.
Ni msichana mrembo
mtaani. Aliolewa na
Mabavu kwa sababu
alimwokoa.
·
Dutu, Mchawi, Moto, Medza, Mama Tabu, Chinengo,Mama Furaha.
MANDHARI
Ni dhana
inayorejelea wakati na
mahali ambapo kazi
ya kifasihi hufanyika.
Dhana hii huelezea
mazingira ya kijamii
na kielimu wanakojikuta
wahusika wa kifasihi.
Mandhari yaweza kuwa
halisi au ya
kubuni. Katika riwaya
hii mwandishi ametumia
mandhari ya kubuni, kwani
tunamwona mhusika Dzombo
jamii aliyokuwa anaishi
haileweki. Ni ya
dhahania. Badaye Sayari
inampeleka hadi ulimwengu
mwingine usiofahamika kiuhalisia.
Ulimwengu huu sio duniani wala peponi (mbinguni). Huku
ndiko jamii ya
walenisi
walikoishi,(ulimwengu huru).
MATUMIZI YA
LUGHA
Mwandishi ametumia
lugha ya kawaida, nyepesi inayoeleweka
kwa msomaji. Lugha
yenye kujaa misemo, methali, tamathali za
semi, mbinu nyingine za
kisanaa na taswira.
Pia ametumia lugha
ya kiingereza kwa
kiasi kidogo.
METHALI NA
MISEMO
·
MISEMO
Misemo iliyotumika
katika riwaya hii ni
-
Mwenye
nguvu mpishe (uk.71)
-
Dunia
mti mkavu (uk.71)
-
Mungu
hana kipimo (uk.77)
-
Kuuliza
si ujinga (uk.83)
-
Panapo
tajiri sharti masikini
awepo (uk.84)
-
Kilimo
cha kufa na
kupona (uk.115)
-
Hebu
fanya fujo uone (uk.188)
-
Usimwamshe aliyelala
ama utalala mwenyewe (uk.191)
·
METHALI
Katika riwaya
ya Walenisi methali
zilizotumika ni kama
vile;
- Kidole
kimoja hakivunji chawa (uk.200)
- Mwerevu
hajinyoi kwa sababu
werevu mwingi huondoa
maarifa (uk.193)
- Fahali
wawili hawakai zizi
moja (uk.173)
- Kilicho
na mwanzo hakikosi
kuwa na mwisho (uk.193)
·
LUGHA YA
KIINGEREZA
-
“Yes”
(uk.75)
-
“I
am sorry” (uk.75)
-
“Shit
Nigger” (uk.31).
TAMATHALI ZA
SEMI
Ni mbinu
ambayo hutumiwa kuelezea
fungu la neno
au maneno ambayo
yamegeuzwa maana yake
asilia na kuwa
na maana nyingine.
Tamathali za semi
zilizotumika katika riwaya
hii ni kama
hizi zifuatazo.
·
TASHIBIHA
Ni tamathali
ya semi ambapo
vitu viwili hulinganishwa
kwa njia wazi
kwa kutumia viunganishi
kama vile “kama”, “mfano wa”, “mithili
ya”, n.k. Tashibiha zilizotumika
ni kama;
- Moyo
ukawa umepoa kama
upoaji wa kutandazika
kwa ulimwengu huu
mpya aliokuwa akiushuhudia. (uk. 36).
- Joho
lake la Hariri
lilikuwa hafifu lilomganda
mithili ya ndizi
na ganda lake (uk.49).
- Matambara
yangu haya huyaona
kama suti (uk. 74)
- Aliondoka
kama vile jibwa
lifanyavyo baada ya
kumwagiwa maji (uk.70).
- Kiwiliwili
chake kilionekana tuli mithili ya
maji ya mtungini (uk. 125).
- Mapenzi
yako yatendeke duniani
kama yatendekavyo mbinguni. (uk.147).
·
TASHIHISI
Ni kitendo
cha kuvipa uwezo
wa kutenda mambo
vitu visivyo na uwezo kama
mwanadamu atendavyo. Mfano.
-Uso wake
ulianza kunawili kwa
tabasamu (uk.41).
-Utambi uliitikia
busu la moto (uk.72).
-Mahindi nayo
yalijianika kama askari
wanaongojea kukaguliwa (uk.113).
·
SITIARI
Hii ni
hali ya kulinganisha
vitu bila kutumia viunganishi.
Mfano:
-Binadamu asiye na utu
ni joka(uk.129)
-Mkataa mtoto ni mchawi
(uk.150)
-Kwenu wake
ni maua (uk.135)
·
TAFSIDA
Ni hali
ya kupunguza ukali
wa maneno. Maneno yasiyopendeza kwa
kutamkwa wazi wazi, hutamkwa kwa kificho.
Mfano:
-Alimsikia Tabu akikata
roho mgongoni mwake (uk.185)
-“Sina kazi
au……..Natafuta kazi ama! Nataka
waandikwe kazi! au nimefutwa
kazi”.Lilichukuliwa kama jambo
kubwa la kujidharau na
kutia haya mithili
ya mtu kwenda
haja hadharani .(uk111)
·
TASHTITI
Ni mshikilio wa jambo kwa kuchagiza
mtu au kwa kuchagiza
kero.
Mfano:-Mabavu
siku moja akamuuliza Kadzo “Vipi
huna macho?” Kadzo akajibu
“Hujayaona?”(163).
-Ni wewe mwanamke ndiwe…………?(uk97)
MBINU NYINGINE
ZA KISANAA.
·
MDOKEZO
Ni
hali ya
kusema maneno bila
kuyamalizia. Maneno haya
yanaweza kumaliziwa na
mtu mwingine au yasimaliziwe kabisa.
Mfano:-Ooo…….Fii…….. usiniache …….usiniache
tafadhali ,Fii…… Fii……..nakupenda sana….nakuu ……(uk.135)
-Miimi…..si sii…..Mungu…. na wala duniani
haa….kuna Mungu (uk.195)
·
TAKRIRI
Ni kitendo cha
kusema jambo moja
kwa kurudiarudia ili kuonesha
msisitizo.
Mfano:-
-“Dzombo kufa !”
“Sifi ng’o!”
“Kufa mwanaharamu wee!”
“Sifi ng’o!”
“Shiit….kufa shenzi wee!”
“Sifi ng’o!”! (uk.32)
-Mimi niko huru, Mimi ni huru, Mimi
niko huru (uk.29)
·
NIDAA
Ni mbinu ya kisanaa inayokuwa
na alama ya mshangao.
Mfano:-Wangejua!! (uk.80)
-Salalaa…..!uuuii!(uk.1)
-Dunia mti mkavu! (uk.71)
·
TANAKALI SAUTI
Ni mwigo
au mlio wa
sauti ya kitu
fulani.
Mfano:-Sayari ikawa
inavuma tu shwaa…..(uk.11)
-Bu! Bu! Bu! (uk.30)
-Tumbo
kugeuzwa na kuwa
gunia la migumio
korokoroo…shoo…buumm! (uk.56)
-Usitupigie
kelele hapa! Pa! kofi
(uk.179)
MATUMIZI YA
LUGHA YA PICHA
(TASWIRA)
Ni mbinu
ya kisanaa ambayo
msanii hutumia lugha ya
kifasihi au picha
zaidi kuashiria kitu
fulani.
Mfano:- Jehanamu-Duniani
-
Walenisi –Ulimwengu huru (ulimwengu
mpya usio na karaha
-
Chembechembe za sukari
-chembechembe za ukombozi .
- Popo -Viongozi
wabaya wasio simamia
upande wowote .
- Majabali
-Matatizo mbalimbali yanayokumba jamii.
Mfano. Jabali la ujinga,
jabali , la mgonjwa.
MCHANGO WA
MWANDISHI KATIKA JAMII
NA WAANDISHI WACHANGA.
Mwandishi ametoa
mchango mkubwa katika
jamii kwa kuonesha na
kuyafikisha maudhui yake
katika jamii. Vilele
mwandishi ameweza kuonesha
vipengele mbalimbali vya
kifani ambavyo wasanii
wachanga hawana budi
kuviiga na kuvitumia.
Mfano, mtindo, muundo matumizi
ya lugha na
vinginevyo.
Pia
mwandishi amewaunda wahusika
kulingana na uhusika
wao. Mfano, Masikini
Jeuri alikuwa mtu mwenye
kuto kuumizwa na
umasikini wake. Wahusika
wengine ni kama
vile Mtu -Binti
Fikirini, Mtu –Binti Hekima ,Mtu
-wazo, Mama -mtu
Maanani na wengine
ambao wamepewa majina kulingana na
uhusika wao.
KUFAULU
NA KUTOFAULU KWA MWANDISHI
KIFANI NA KIMAUDHUI.
(a)
KUFAULU
Mwandishi
amefaulu kimaudhui kwa kufikisha
ujumbe na dhamira
yake kwa jamii/ulimwengu aliokusudia.
Ameonesha wazi mbinu za
ujenzi wa jamii mpya
kuwa ni kuamka
na kuwa na
ufahamu juu ya wanyonyaji
na kupambana na
unyonyaji huo.
Mwandishi pia
amefaulu kifani ,kwani ametumia
lugha nyepesi inayoeleweka
kwa wasomaji. Pia amewajenga
wahusika wake vizuri
kulingana na uhusika
wao . Amefaulu pia
kwa kujenga jina
la kitabu linalosadifu
yale yaliyomo ndani.
(a)
KUTOFAULU.
Kimaudhui mwandishi
hajafanikiwa kwa kutokuonesha
nini kilitokea baada Dzombo
kurudi duniani. Kifani
mwandishi ameshindwa, kwani ametumia mandhari
isiyoeleweka kuwa Walenisi
wanaishi ulimwengu gani,
kitu ambacho pia
humchanganya msomaji.
JINA LA
KITABU
Jina la
kitabu “Walenisi” linasadifu
na kusawiri yale yaliyozungumzwa ndani
ya kitabu hiki.
Jina la WALENISI
lilitokea baada ya
ulimwengu wa wachuna uliojulikana
kwa jina la
WALENI (“Wale na
waliwe”) kupinduliwa na
hatimaye jina hili
kubadilka na kuwa
ulimwengu wa “WALENISI” ,ikimaanisha, “Wale
ni sisi na
sisi tu wale…….walenisi” Yaani umoja usiobadilika . (uk.195).Mwandishi katika
wimbo ulioimbwa na
vijana wa kiwalenisi
ansema, “Walenisi ni
sisi”
“Warithi
wa usisi”
“Yule nawe
tu sisi”
“Tu sisi
ni walenisi”. (uk.113)
HITIMISHO
Kwa kuhitimisha,
mwandishi wa riwaya
ya Walenisi anaelezea
mambo mbalimbali yaliyokuwa
yakifanywa na jamii
ya wachuna ambayo
pia yanafanyika katika
jamii zetu. Ameonesha
pia mambo yaliyokuwa
yakifanywa na Walenisi
ambayo jamii zetu
hazina budi kuyaiga
na kubadilika, na hatimaye
kuishi maisha mazuri
kama waliyokuwa wakiishi
Walenisi.
Maoni
Chapisha Maoni