Kazi
hii inahusu uchambuzi wa maudhui katika riwaya ya mkondo wa kipelelezi na
kiarifu ambayo inaitwa “Tutarudi na Roho
Zetu?”iliyoandikwa na Ben Mtobwa. Katika kujadili riwaya hii tutaeleza
dhana ya riwaya, dhana ya mkondo wa kipelelezi, usuli wa mwandishi, muhtasari
wa kitabuchenyewe, nadharia itakayotumika kuchambua maudhui ya kitabu hiki,
uchambuzi wa maudhui na hitimisho.
1.1 Dhana ya Riwaya
Kwa
mujibu wa Madumulla (2009) akimrejelea Msokile (1992) anafafanua kuwa riwaya ni
kazi ya sanaa ya kubuni, ni maandishi ya nathari (ujazo) yanayosimulia hadithi
ambayo kwa kawaida ina uzito, upana, urefu wa kutosha, ina wahusika wengi wenye
tabia mbalimbali, ina migogoro mingi mikubwa na midogo.
Senkoro
(1982) anasema riwaya ni hadithi ndefu ya kubuni yenye visa vingi, wahusika
zaidi ya mmoja, na yenye mazungumzo na maelezo yanayozingatia kwa undani na
upana maisha ya jamii.
Wamitila
(2003), Samwel na wenzake (2013), wanasema kuwa riwaya ni kazi andishi ya
fasihi ambayo kwa kawaida ni ndefu zaidi kuliko hadithi fupi. Urefu wa riwaya
maana yake ni kwamba msuko simulizi umejengeka vizuri, kuna wahusika wengi,
inaenea muda mrefu, na mada zake ni nzito na pana kiasi. Mifano mizuri ya
riwaya kwa lugha ya Kiswahili ni “Nagona”
au “Mzingile” riwaya za mwandishi
Euphrase Kezilahabi.
Kwa
ujumla riwaya ni hadithi ndefu za kubuni zenye wahusika wengi au wachache
zinazoelezea maisha ya mtu au jamii fulani.
1.2 Dhana ya mkondo wa kiarifu na
kipelelezi
Kwa
mujibu wa Madumulla (katajwa) mkondo
wa kiarifu na kipelelezi ni kategoria ya ubunaji kuhusu uhalifu na upelelezi
iliyojitokeza katika fasihi ya Kiswahili karibu mwishoni mwa muongo wa hamsini
wa karne ya 20.
Mkondo wa
kipelelezi; aina hii ya utunzi inahusishahadithi zinazosimulia kuhusu
upeleleziwa uhalifu fulani kama vileujambazi, wizi, rushwa, mauaji. Kwakawaida
huanza na tukio fulani la uhalifu ambalo limekwisha tendekanaye msimulizi
huwaongoza wasomajikatika safari ya kung'amua kiini chauhalifu husika. Sifa kuu
ya hadithihizi ni kwamba husheheni taharukinyingi na huiteka hadhira kwa
kuchocheahamu ya kugundua au kuteguakitendawili. Kwa mfano riwaya ya'Masaibu ya
Ndugu Jero.' (Taifa leo, 2015).
Hivyo
basi mkondo wa kiarifu na kipelelezi ni mkondo ambao unahusu riwaya zenye
uhalifu na upelelezi ndani yake kama vile ujambazi, rushwa na mauaji. Kwa mfano
katika riwaya hii ya “Tutarudi na roho
zetu?” ni mfano mzuri wa mkondo huu kwani umejaa upelelezi na uhalifu ndani
yake.
1.3 Usuli wa Mwandishi
Kwa
mujibu wa Dr. Mikhail (2008) mwandishi Ben Rashid Mtobwa alizaliwa tarehe
28 mwezi wa nane, mwaka 1958 huko mkoani
Kigoma, magharibi ya Tanzania. Maisha yake na kazi yake alijikita katika
uandishi kwa lugha ya Kiswahili. Alioa na alikuwa na watoto wanne.
Ben
Mtobwa alianza uandishi akiwa shule ya sekondari. Baadaye alianza kuandika
habari katika magazeti kama “Nchi yangu,”
“Bara Afrika” na “Kiongozi”. Pia, uhariri katika magazeti
kama “Uhuru na Mfanyakazi”. Akiwa
mwandishi alianza kujulikana miaka ya 1980 akiwa miongoni mwa waandishi
walioanza kuandika vitabu vya Kiswahili. Vitabu vyake vilivyojulikana sana
miaka hiyo ni “Dimbwi la Damu” (1984),“Tutarudi
na Roho zetu?” (1984), “Najisikia
Kuua Tena” (1985), “Joram Kiango
Mikononi mwa Nunda” (1986),Lazima Ufe
Joram” (1986), “Pesa Zako Zinanuka”
(1986),“Salamu Kutoka Kuzimu” (1987),
“Malaika wa Shetani” (1988),Dar es Salaam Usiku” (1990), “Zawadi ya Ushindi” (1992), “Nyuma ya Mapazia” (1996), “Roho ya Paka” (1996) “Mtambo
wa Mauti” (2004). Piaaliandika kitabu cha watoto kilichoitwa “Nitakusubiri” na habari ndogo iliyoitwa
“Mwanaharamu”na mwishoni kabla ya
kifo aliandika kitabu kilichoitwa “Mikataba
ya Kishetani”.
Baada
ya kujulikana kama mwandishi miaka ya 1980 Ben Mtobwa alikuwa meneja mwongozaji
katika kampuni ya uchapishaji ya Heko iliyopo jijini Dar es Salaam. Baadae
kampuni hiyo ilikuwa muhimu sana katika usambazaji wa vitabu vya fasihi,
uchapishaji wa magazeti na kuwasaidia waandishi chipukizi.
Ben
Mtobwa alifariki tarehe 9/11/2008, akiondoka na mipango mingi mipya na matumaini
makubwa katika kuikuza fasihi na maisha ya jamii. Hali hii imezifanya jamii
kumkumbuka sana kutokana na mchango wake kiuandishi na kifasihi.
1.4 Muhtasari wa kitabu
“Tutarudi na Roho Zetu?” ni riwaya iliyoandikwa na Ben
Mtobwa. Riwaya hii inaelezea shughuli zilizofanywa na nchi za mstari wa mbele
katika ukombozi kusini mwa Afrika, zimetendwa mengi maovu na utawala
dhalimu….hata hivyo haikupatikana kutokea tishio zito la kutisha kama hili,
ambalo linakaribia kutokea. Tukio la kutatanisha ambalo linawatoa machozi
wananchi wanchi mbalimbali. Wanajitokeza mashujaa kwenda Afrika kusini, lakini
kila aendaye huko harudi na roho yake.
Inspecta
Kombora nchiniTanzania jasho linamtoka. Anawathamini mashujaa wengi lakini
anamtambua shujaa mmoja Joram Kiango. Jambo la kusikitisha ni kwamba sasa hivi
Joram ni mtumiaji mzuri ambaye anatembea kutoka jiji hadi jiji akiwa na yule
msichana mzuri Nuru. Juhudi za Kombora kumsihi hazikufua dafu. Badala yake
Joram anafanya maajabu mengine ambayo yanalichafua jina lake hapa nchini na
kote duniani. Wakati huo siku ambayo utawala huo umeweka ili kuachia pigo lao
la mwisho inazidi kukaribia. Sasa yamesalia masaa, lakini baadae Joram
anaonekana ndiye mkombozi mkuu wa nchi za mstari wa mbele. Mwandishi wa hadithi
hii amezungumzia mambo tofauti tofauti kwa zana mbalimbali ambazo ni pamoja na
watu wenye bahati na wenye mikosi, wasichana wenye sura nzuri na wale wenye
mbaya. Ni hadithi kuhusu mapenzi na chuki, uhai na kifo.
1.5 Nadharia ya Uhalisia
TUKI
(2004) wanaeleza kuwa nadharia ni mawazo, maelezo na muongozo uliopangwa ili
kusaidia kuelezea kutatua au kutekeleza jambo fulani. Nadharia yoyote ile ya
kihakiki ni nyezo ya kusaidia kufikisha lengo fulani.
Kwa
mujibu wa Ntarangwi (2004) anasema nadharia ya uhalisia ni uwakilishi wa
uhalisi wa mambo katika fasihi, nadharia hii ilizuka katika karne ya 19
hususani kwa sababu za kupinga mkondo wa ulimbwende.
Hivyo basi, nadharia ya uhalisia ni nadharia
ambayo hujikita katika mambo yaliyopo, tukio mahususi na matokeo yanayoweza
kuthibitika. Tukirejelea katika riwaya ya “Tutarudi
na Roho Zetu?”mwandishi amejikita katika uhalisia kwani amezungumzia mambo
ambayo yanajitokeza na yapo katika jamii. Hivyo tutatumia nadharia hii kuhakiki
maudhui yaliyojitokeza katika kitabu hiki kwa kuwa kitabu hiki kinasawiri mambo
ambayo yapo katika jamii zetu.
2.0 Maudhui katika Riwaya ya “Tutarudi na Roho Zetu?”
Kwa
mujibu wa Madumulla (katajwa) maudhui
ni mawazo fikra na ujumbe uliomo katika kazi ya fasihi.Maudhui ina vipengele
mbalimbali ambavyo ni pamoja na dhamira, ujumbe, falsafa, migogoro, msimamo na
mtazamo wa mwandishi. Katika riwaya ya “Tutarudi
na Roho Zetu?” vipengele vya maudhui vinavyojipambanua au kujidhihirisha ni
pamoja na:-
2.1 Dhamira
Madumulla
(katajwa) anasema dhamira ni wazo kuu
katika kazi ya fasihi. Dhamira ni sehemu tu ya maudhui. Dhamira ndiyo hujenga
kiini cha kazi ya fasihi,yafuatayo ni mawazo au dhamira zilizojitokeza katika
riwaya hii ya “Tutarudi na Roho Zetu?”
2.1.1 Ukombozi
TUKI
(katajwa) wanasema kuwa ukombozi ni
uokoaji wa watu kutoka kwenye hali mbaya ya udhalimu au hali duni. Katika
riwaya hii kuna aina mbili za ukombozi zilizojitokeza ambazo ni ukombozi wa
kisiasa na ukombozi wa kifikra.
2.1.1.1Ukombozi wa Kisiasa
Katika
riwaya ya “Tutarudi na Roho Zetu?”miongoni
mwa ukombozi uliojitokeza ni ukombozi wa kisiasa. Mwandishi anadhihirisha
ukombozi wa kisiasa kwa kumtumia mhusika wakemkuu Joram ambaye ni mpelelezi,
analisaidia bara lake kupata ukombozi kutoka katika mikono ya makaburu akishirikiana
na mwenzake Nuru. Mwandishi anasema;
“Kwa kila hali inaonyesha dhahiri
kuwa Joram Kiango akishirikiana na mwenzi wake, yule msichana mzuri Nuru.
Wameshiriki kwa njia moja au nyingine katika kufanya hayo yaliyofanyika huko
Afrika Kusini.Na endapo wasingefanya walichokifanya dakika hii hii Afrika nzima
ingekuwa katika msiba kwani kulikuwa na mipango ya mtambo huo kuzishambulia
nchi zote za mstari wa mbele kwa pamoja”(uk
173).
2.1.1.2 Ukombozi wa Kifikra
Mwandishi anaonesha ukombozi wa kifikra katikariwaya
hii kwa kumtumia mhusika wake Joram.Pale ambapo Joram aliamua kurudi tena na
kupigania ukombozi katika bara lake, baada ya kukaa muda mrefu akiwa anastarehe
na Nuru katika miji mbalimbali na baadaetunaona jinsi anavyojitoa kusaidia bara
lake kwa kutega vigololi vilivyopatikana kwa Chonde na kuvitega katika majengo
muhimu ya Makaburu wa Afrika kusini kwa muda wa masaa machache.Mwandishi
anasema;
“Wakiwa wameikariri ramani hiyo
kikamilifu kazi waliyoifanya mitaani humo ilikuwa ya kufuata yale majengo waliyokusudia
na kutega vile vigololi vilivyopatikana kwa chonde na kuvitegesha katika
kipindi cha saa tatu kamili”(uk 132).
Katika
jamii yetu suala la ukombozi limejitokeza hasa kipindi kilichopita cha
uchaguzi, watu wengi wamekombolewa kifikra katika suala zima la siasa, ambapo
imepelekea wanajamii (watanzania) wengi kujiingiza katika siasa na kutafuta
haki ndani ya siasa.
2.1.2 Kujitoa mhanga
Kujitoa
mhanga ni kufanya jambo fulani kwa ajili ya kitu, mtu au watu fulani na kuwa
tayari kwa lolote (www.merriam-webster.com/dictionary/sacrifice).Katika
riwaya ya hii tunaona suala la kujitoa mhanga limejitokeza, kwani tumeona jinsi
Joram na Nuru wanavyojitoa ili kuikomboa nchi yao, hadi kufikia hatua ya
kuhatarisha uhai wao na hata wao wenyewe kuua ili tu waweze kulikomboa bara lao
dhidi ya makaburu. Mwandishi anadhihirisha suala la kujitoa mhanga kwa kumtumia
mhusika wake Nuru alivyojitoa mhanga na kumuua Chonde kwa bastola ili kuokoa
maisha ya Joram. Mwandishi anasema;
“Risasi mbili tatu zaidi zilisikika
kama zilizopigwa bila shabaha yeyote. Kisha kimya kikafuata, kimya ambacho
kilitoweka kwa mkoromo wa mtu aliyekuwa akikata roho………….” (Uk 47)
Vile
vile mwandishi ameonyesha suala la kujitoa mhanga kwa kumtumia mkaburu
aliyetoka Afrika kusini kuja Tanzania kwa lengo la kufanya upelelezi huku akiwa
amefanya plastic surgery miaka 10 iliyopita, ambapo tumboni alionekana mweusi,
usoni na mikononi alikuwa mweupe ili hali yeye kwa asili ni mtu mweupe,hii
inathibitisha jinsi mkaburu huyo alivyojitoa mhanga ili aweze kupata taarifa
kutoka katika nchi ya Tanzania. Mwandishi anasema;
“………….Ningependa
ieleweke kuwa mimi siyo mzungu…..mimi ni mtu mweusi mzaliwa wa Soweto ….. Ngozi
hii nyeupe iliyokaa usoni na mikononi ni matokeo ya plastic surgery ambayo
niliifanya miaka kumi iliyopita.” (Uk 95)
Katika jamii tunayoishi suala la kujitoa mhanga limejitokeza
kwani tunaona baadhi ya viongozi walivyoamua kujitoa mhanga ili kuleta
maendeleo katika jamii.
2.1.3 Ujasiri
Kwa
mujibu wa TUKI (katajwa) ujasiri ni
hali ya kukabili jambo bila ya hofu, uhodari na ushujaa. Katika riwaya hii
mwandishi ameonesha suala la ujasiri kwa kuwatumia wahusika wake wakuu Joram na
Nuru. Ujasiri umejitokeza kwa kiwango kikubwa kwani tunaona jinsi Joram na Nuru
walivyokuwa jasiri katika harakati za kulikomboa bara lao kutoka katika mikono
ya makaburu watu ambao waliwafanyia maovu mengi. Mwandishi anasema;
“Lazima tupambane nao, na huu ni
wakati pekee wa kuonyesha moyo wetu. Uoga hauwezi kutufanya tukubali kuwa
mateka wa utawala haramu kama huu. Lazima tushinde” (Uk 93).
Vilevile
tunaona jinsi Joram alivyokuwa jasiri kujibu swali aliloulizwa na Nuru kuhusu
wizi alioufanya katika City drive bank. Joram alimjibu kwa ujasiri kuwa ameiba
ila ameiba waziwazi tofauti na wenzake wanaoiba kwa siri na kufanya maendeleo
ambayo hayaendani na mishahara yao. Mwandishi anasema;
“Huoni watu wenye mishahara ya
shilingi elfu mbili wanavyojenga majumba ya mamilioni? Unadhani wanazipata wapi
bila wizi? Tofauti yangu na wao ni kwamba mimi nimeiba machomacho, wao wanaiba
kusirisiri. Mwizi ni mwizi tu” (uk 65).
Pia tunaona jinsi Nuru alivyoonesha ujasiri
wake kwa kumuua Iron Von baada ya kumteka Nuru kwa nia ya kutimiza haja yake ya
mapenzi, na kumwonesha alipo Joram na baada ya hapo amuue. Mwandishi anasema;
“Pokea chako, muuaji mkubwa” Nuru
alinong’ona na akiifyatua bastola” (uk 159).
Hivyo,
katika jamii yetu suala la ujasiri linajidhihirisha wazi kwani tunaona jinsi baadhi
ya wanajamii walivyofanya matendo ya kijasiri katika kufichua ubadhilifu
unaofanywa na watu wachache katika jamii ili kuikomboa jamii yao au nchi yao.
2.1.4 Uzalendo
Kwa
mujibu wa TUKI (katajwa) uzalendo ni hali ya mtu kuwa tayari kuifia nchi yake.
Katika kuchambua riwaya hii ya “Tutarudi
roho zetu?” Suala la uzalendo limejipambanua vyema, mwandishi anathibitisha
suala la uzalendo kwa kuwatumia wahusika wake Joram na Nuru ambao wameonesha
uzalendo mkubwa kwa kuipenda nchi yao kwa dhati hadi kuchukua jukumu la
kupambana na kuwaua makaburu ambao wamewatesa kwa muda mrefu kwa lengo la
kuikomboa nchi yao kutoka katika mikono ya makaburu. Mwandishi anasema;
“Nadhani inatosha. Wanakufa wenye
hatia na wasio na hatia sasa iliyobaki ni ile kazi moja ya mwisho kulipua huo
mtambo” (Uk 34).
Vilevile,
suala la uzalendo linajidhihirisha kwa mhusika inspecta Kombora. Matendo yake
yalikuwa ya kizalendo kwa nchi yake kwani alitumia mbinu mbalimbali ya
kupambana na kuwaondoa makaburu wa Afrika Kusini. Mwandishi anasema;
“Kombora alikuwa mwenyeji, alikuwa
mwenyekiti wa mkutano huo ambao ulifanywa kwa siri kubwa mkutano ambao
ulijumuisha watu wenye sura mbalimbali, umri mbali mbali, viwango mbali mbali
vya elimu wote wakiwa na dhamira moja” (uk 94).
Pia,
Inspecta Kombora amedhihirisha uzalendo pale ambapo aliamua kubaki ofisini
baada ya wenzake kuondoka na kwenda kujumuika na familia zao hadi dakika ya
mwisho na kushindwa kwenda kujumuika na familia yake ili aweze kuona nini
kitatokea. Aliamua kukubaliana na tendo lolote ambalo lingetokea pale. Kwani
kutoka muda mfupi uliopita walikuwa tayari wameshapata taarifa kutoka katika
kibarua kilichokutwa ikulu kuwa baada ya masaa 3 kungetokea mlipuko katika
maeneo hayo. Mwandishi anasema;
“Alikuwa
ameamua lolote ambalo lingetukia, limkute katika ofisi yake” (Uk 171).
Katika
jamii zetu suala hili la uzalendo linajidhihirisha wazi kwani tunaona jinsi
baadhi ya viongozi wanavyojitoa katika nchi hii kwa namna moja au nyingine. Kwa
mfano, tunaona baadhi ya viongozi wa kisiasa walivyoonesha uzalendo katika nchi
yao kwa kukataa kulipwa hela za ziada au posho za vikao kwa kuona kuwa siyo
haki yao bali ni ubadhilifu na kuwanyonya wananchi.
2.1.5Ubaguzi wa rangi
Ubaguzi
wa rangi ni ile hali au kitendo cha kuwaweka watu katika makundi kutokana na
rangi zao kwa ajili ya kutoa huduma tofauti tofauti kulingana na rangi zao. (https://en.wikipedia.org/wiki/Racial_discrimination).Suala
la ubaguzi wa rangi limejitokeza katika riwaya hii ambapo inaelezwa kuwa watu
wa rangi nyeusi wanatazamwa kuwa ni watu wenye fikra ndogo, wasiokuwa na akili
ambao hawawezi kuleta maendeleo yoyote zaidi ya mtu mweupe. Na pia wanathubutu
kusema kuwa ngozi nyeusi ni dalili ya laana ambapo mtu huyu mweupe ndiye
anaonekana mwenye akili. Mwandishi anasema;
“Ngozi nyeusi ni dalili ya laana. Nywele fupi nidalili ya
akili ndogo. Bila hekima uongozi wa mtu mweupe Afrika ingekuwa bado gizani, na
endapo ataondoka mtu mweupe giza litarudi”(uk 104).
2.2 Migogoro
Kwa mujibu wa TUKI(katajwa)wanasema kuwa migogoro ni hali ya kutofautiana baina ya
pande mbili au zaidi, wanasema migogoro inaweza kuwa ya familia, matabaka ya
kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. Katika riwaya hii imejitokeza migogoro tofautitofauti
kama ifuatavyo:
2.2.1 Mgogoro kati ya makaburu
(wazungu) na watu weusi
Mgogoro
huu ulitokea wakati watu weupe (makaburu) wakiwadharau watu weusi na kuwaona si
chochote, watu duni pamoja na kuwafanyia maovu mengi. Mgogoro umesababishwa na
tofauti za rangi na kupelekea uadui mkubwa kati ya watu weupe na weusi. Ubaguzi
huu wa rangi ambao ulisababishwa na siasa ya magharibi ndio uliopelekea
mapigano kati ya watu weupe na weusi na kupelekea vifo hasa kwa watu weusi.
Yote haya yamejidhihirisha kwa mawanda mapana katika riwaya hii (uk 104).
2.2.2 Mgogoro kati ya Inspecta
Kombora na Joram Kiango
Mgogoro
huu ulitokea pale ambapo Inspecta alipomfuata Joram na kumsihi arudi katika
kazi yake ya upelelezi. Na Joram kukataa ombi hilo. Suluhisho ni pale ambapo
Inspecta Kombora aliamua kuondoka (uk 19).
2.2.3 Mgogoro kati ya Nuru na Joram
Mgogoro
huu ulitokea wakati Nuru akimbembeleza sana Joram arudishe pesa alizoiba kutoka
katika Benki ya City Drive. Pamoja na kwenda kuomba msamaha ubalozini na Joram
kutokubaliana naye kwa wakati ule. Suluhisho ni pale ambapo baadae alikubali
kurudisha pesa zile Benki baada ya kulipua mji wa Soweto uliopo Afrika kusini
japokuwa hakupenda kwenda kuomba msamaha ubalozini (uk 66).
2.2.4 Mgogoro wa nafsi
Huu
ni mgogoro unaojitokeza baina ya mtu mmoja ndani ya nafsi yake. Katika riwaya
hii mgogoro wa nafsi umejitokeza kwa Joram pale ambapo alitoka kuongea na
Chonde na baadaye akaanza kujiuliza kuwa huyu ni mtu wa aina gani na amelijua
vipi jina langu? (uk 25).
2.3 Ujumbe
Kwa
mujibu wa Madumulla (katajwa)ujumbe
ni kitu ambacho mwandishi hudhamiria kumtumia msomaji, kila kazi ya fasihi
hubeba ujumbe ambao msanii hutaka umfikie msomaji wake.Katika riwaya ya hii
kuna ujumbe wa aina tofauti tofauti uliojitokeza kama ifuatavyo:
2.3.1Kujitoa
mhanga ni njia mojawapo ya kupata ukombozi katika harakati za kudai uhuru
mwanamke hapaswi kuachwa nyuma kwani ana mchango mkubwa ambao unapelekea
ukombozi.
2.3.2
Ujasiri ni muhimu katika harakati zote za ukombozi.
2.3.3Uzalendo
ni muhimu katika harakati za kutafuta ukombozi, mwananchi lazima awe mzalendo
na nchi yake.
2.3.4Ubaguzi
wa rangi ni kikwazo ambacho kinapelekea uadui mkubwa baina ya nchi na nchi.
Hivyo hatuna budi kufuatilia mbali ubaguzi wa rangi.
2.3.5
Katika harakati za kudai uhuru mwanamke mwanamke hapaswi kuachwa nyuma kwani
ana mchango mkubwa ambao unapelekea ukombozi.
2.4Falsafa
Kwa mujibu wa Madumulla(katajwa)akimrejelea Msokile (2009) falsafa ni wazo ambalo mtu
anaamini kuna ukweli fulani unaohusu maisha yake pamoja na maisha ya
jamii.Katika riwaya ya hii mwandishi anaamini kuwa ili kufanikiwa katika suala
zima la ukombozi ni lazima tujitoe mhanga tuwe na ujasiri pamoja na uzalendo
kwa kile tunachotaka kukikomboa.
2.5Msimamo
Kwa mujibu wa Madumulla (katajwa) ni mawazo, mafunzo na falsafa ya msanii. Hubainisha
msimamo wake kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii na ndiyo huweza
kuwatofautisha wasanii wawili au zaidi wanaoandika kuhusu mazingira
yanayofanana. Katika riwaya hii mwandishi ana msimamo wa kimapinduzi kwani
ameonesha kuwa mtu kuwa na ujasiri, kujitoa mhanga pamoja na uzalendo ni silaha
kuu katika kuleta ukombozi.
3.0 Hitimisho
Kwa
ujumla riwaya hii ya “Tutarudi na Roho
Zetu?”inaelezea namna nchi za mstari wa mbele zilivyoshikamana ili kupinga
na kupambana na makaburu huko Afrika ya Kusini waliowatenda maovu watu weusi na
kuwachukulia kama watu wasio na akili na hatimaye watu weusi kufanikiwa
kuwashinda makuburu kutokana na juhudi kubwa zilizoongozwa na Joram Kiango.
4.0 Marejeo
Gazeti la Taifa Leo,
(15-10-2015),Jumatano.
Kezilahabi,
E. (1991), Mzingile,University of Dar
es Salaam Press; Dar es Salaam.
Kezirahabi,
E. (1990), Nagona, University of Dar
es Salaam Press; Dar es Salaam.
Madumulla, S.J (2009), Riwaya ya Kiswahili, Nadharia,Historia na Misingi
ya Uchunguzi.
Mture Educational Puplishers Limited; Dar-es salaam.
Mikhail,
G. (2008), Swahili Forum 15. United
States International University; Nairobi.
Msokile, M. (1992) Kunga za Fasihi na lugha.Educational
Publishers and Distributors, Limited; Dar es Salaam.
Mtobwa, B. (2008), Tutarudi na Roho Zetu?. East Africa
Educational Publishers LTD; Dar es Salaam.
Ntarangwi, M. (2004), Uhakiki wa Kazi za Fasihi.
Samwel, M. na Wenzake (2013) Ushairi wa Kiswahili, Nadharia, Mifano na
Muongozo kwa Walimu wa Kiswahili. MEVELI Publishers; Dar es Salaam.
Senkoro, E.(1982), Fasihi. Press and Publicity Centre; Dar-es-Salaam.
TUKI
(2004), Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Oxford
University Press; Dar es Salaam.
Wamitila na Kyallo,W. (2003), Kamusi ya Fasihi Istilahi na Nadharia,
Focus Publications; Nairobi.
www.en.wikipedia.org/wiki/Racial_discrimination
16:59 on 22nd Dec. 2015
www.merriam-webster.com/dictionary/sacrifice 17:15 on 22nd Dec. 2015
Maoni
Chapisha Maoni