USHAIRI
Kuna
mitazamo ya aina mbili katika kuelezea dhana ya ushairi. kuna wanamapokeo na
mamboleo. Hata hivyo kabla ya kuendelea zaidi kuwachambua tuangalie wataalam
mbalimbali wanavyofasili dhana hii . Dhana ya ushairi imejadiliwa na wataalamu
mbalimbali huku kila mmoja akitoa fasili yake. Baadhi ya wataalam hao ni kama
ifuatavyo:
MAPOKEO
Mssamba, (2003) akimnukuu Shaban Robert, anasema;
“ushairi ni sanaa ya vina inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi zaidi
ya kuwa na sanaa ya vina ushairi unaufasaha wa maneno machache au muhtasari.”
Mnyampala
(1970) anasema kuwa “ushairi ni msingi wa maneno ya hekima tangu kale ndicho
kitu kilichobora sana maongozo ya Dunia kwa kutumia maneno ya mkato na lugha
nzito yenye kunata iliyopangwa kwa urari wa mizani na vina maalum.”
Amri
Abeid (1954:1) anasema kuwa “ushairi au utenzi ni wimbo, hivyo kama shairi
haliimbiki halina maana.”
Abdulatifu anasema
kwamba ushairi ni ule ulio na sifa ya ulinganifu wa vina na mizani, lugha laini
(lugha tamu) na lugha hii iweze kugusa moja kama ilivyokusudiwa.
Encyclopedia
American (EA) inaeleza kuwa ushairi ni kauli zenye hisia na ubunifu,
mpangilio fulani wenye urari, uwasilishaji wa tajiriba au mawazo ya mtunzi kwa
maana ambayo huibua tajiriba kama hiyo katika nyayo za wasomaji au wasikilizaji
na kutumia lugha ya picha.
MAMBOLEO
Kezilahabi
( )anasema kuwa “ushairi ni tukio hai au wazo ambalo limeonywa kwetu kutokana
na upangaji uzuri wa maneno fasaha yenye mizani Fulani ili kuonyesha ukweli”
Topan
(1996) anasema kuwa “shairi ni unaoeleza hisia za ndani za binadamu kwa
mpangilio Fulani wa maneno” hivyo kwa mujibu wa Topan ushairi lazima uguse
hisia za ndani ya moyo wa binadamu.
Njogu
na Chimerah (1999) wanasema “ ushairi ni sanaa ya lugha inayoeleza jambo kwa
njia ya mkato na kwa namna inavyoteka hisia za msomaji au msikilizaji”
Mulokozi
na Kahigi (1982:25) wanasema ushairi ni “sanaa inayopambanuliwa kwa mpangilio
maalum na fasaha na wenye muwala, kwa lugha ya picha, sitiari au ishara katika usemi,
maandishi au mahadhi ya wimbo ili kuleta wazo au mawazo, kufunza au kueleza
tukio au hisia fulani kuhusu maisha au mazingira ya binadamu kwa njia inayogusa
moyo.”
Hivyo basi tunaweza kusema kuwa ushairi ni kazi ya
sanaa yenye kuandikwa au kuimbwa kwa kufuata kanuni za ushairi au kutofuata kanuni za ushairi ikiwa na maana kuwa
ushairi waweza kuwa wa kimapokeo au wa kisasa ilimradi ushairi huo uwe na
ujumbe.
Katika ushairi FANI na MAUDHUI ni muhimu sana, mawazo
fikra au sihi za ndani ni vitu muhimu sana katika ushairi
CHANZO/CHIMBUKO LA USHAIRI
Dhana ya chimbuko inafasiliwa na TUKI (2004) kuwa
ni mwazo au asili ya kitu. Baadhi ya wataalamu wameweza kuelezea chimbuko la
ushairi wa Kiswahili kwa kuzingatia mitazamo au nadharia mbili ambazo ni kama
ifuatavyo:
1. Nadharia ya kwanza inadai kuwa;
Chimbuko la ushairi wa Kiswahili ulitokana na ujio wa Waarabu.
2. Na nadharia ya pili inasema kuwa; Chimbuko la
ushairi wa Kiswahili ni zao la jamii ya waswahili wenyewe.
USHAIRI WA KISWAHILI ULITOKANA NA UJIO WA
WAARABU.
Kwa kuanza na Lyndon
(1962) “Swahili Poetry” anatoa hoja tatu ambazo ni:
·
ushairi wa Kiswahili umetokana na Uislamu,
·
ushairi ulianzia kwenye upwa wa kaskazini mwa Kenya
hususani Lamu.
·
Na
maudhui ya ushairi wa Kiswahili yalitokana na ushairi wa Kiarabu. Utungo wa
kwanza wa ushairi andishi wa Kiswahili ni Tambuka, Mwengo bin Athmani (1728)
Ubora wa
Nadharia hii
·
Ubora wa nadharia hii au mtazamo wa Harries
kuhusu chimbuko la ushairi wa Kiswahili ni kwamba umesaidia wengine kuendelea
kuchunguza zaidi kuhusu chimbuko la ushairi wa Kiswahili.
Udhaifu wa
nadharia hii
·
Udhaifu wa nadharia hii ni kuwa si kweli kwamba
ushairi wa Kiswahili uliletwa na Uislamu bali ulikuwepo hata kabla ya ujio wa
Uislamu, kwani ushairi hautenganishwi na jamii husika. Hivyo jamii za waswahili
walitumia Nyanja mbalimbali za ushairi katika shughuli zao mbalimbali au
shughuli zao za kila siku, kama vile; shughuli za kilimo na ufugaji.
·
Pia ushairi wa Kiswahili ulianza karne ya 10BK
na ushairi wa Kiswahili ulikuwa ukitungwa na kughanwa kwa ghibu bila kuandikwa.
Wataalam wengi wanakubaliana kuwa asili ya ushairi wa Kiswahili ni tungo
simulizi hasa ngoma na nyimbo.
·
Udhaifu mwingine katika mtazamo wa kusema kuwa
ushairi ulianzia pwani ya kaskazini ya Kenya si kweli kwa kuwa waswahili
walikuwepo hata sehemu nyingine kama vile Kilwa na Bagamoyo ambapo ushairi wa
Kiswahili ulitumika.
·
Hoja ya kusema ushairi wa Kiswahili ulitokana na
Kiarabu haina mashiko kwa kuwa waswahili walikuwepo hata kabla ya waarabu na
walikuwa na ushairi wao isipokuwa ujio wao ulileta athari kubwa kwa kuwa
ulichanganya na mambo ya dini ya kiislamu na hati.
Knappert (1979)
“Four centuries of Swahili verse” anasema; “Ushairi wa Kiswahili
ulichipuka kwenye upwa wa Kenya kutokana na nyimbo na ngoma za waswahili na
ulianza katika karne ya 17 na pia ni ushairi wa Kiislamu wenye kuchanganya sifa
za tungo za kiafrika na za kiajemi.
Ubora wa hoja
Ubora wa hoja hii
ni kwamba, ni kweli Knappert amekubali kuwa,ushairi wa Kiswahili ulitokana na
waswahili wenyewe.
Udhaifu
wa hoja
Hata hivyo hoja
yake ina udhaifu kwa kuwa ushairi wa Kiswahili ulianza kabla ya karne ya 10 BK
na pia amejikita katika maudhui ya mambo mengine kama vile siasa, uchumi na
kijamii. Vilevile amechanganya chimbuko la ushairi wa Kiswahili na Uarabu.
USHAIRI NI ZAO LA WASWAHILI WENYEWE.
Nadharia hii
imejadiliwa na wataalam mbalimbali akiwemo Shaban Robert, Jumanne Mayoka (1993)
na Senkoro, Mulokozi na Sengo.
Jumanne, M. Mayoka (1993) anasema
ushairi umetokana na jamii ya wanadamu wenyewe na umesheheneza ukwasi mkubwa wa
lugha ambayo imekuwa ikitumika katika hatua zote za kisiasa, kiuchumi na
kiutamaduni katika historia ambayo mwanadamu amepitia, Kwa mfano kwa msamiati
uliotumika tangu enzi za kuishi mapangoni, enzi za uwindaji, ujima, utumwa,
vita vya makabila, uvamizi wa wageni, ukoloni na harakati za kupambana na
ukoloni hadi kupata uhuru na maendeleo yake.
Ubora wa hoja
Ubora wa hoja hii
ni kwamba ina mashiko ndani yake kwa sababu, kila jamii ina sanaa yake na
ushairi ni moja kati ya sanaa hizo ingawa inaweza ikaathiriwa na sanaa ya jamii
nyingine. Pia ushairi umekuwa ukikua na kuendelea kadri jamii inavyokuwa na
kuendelea.
Udhaifu wa
hoja.
Udhaifu wa hoja
hii ni kwamba si kweli kuwa katika kipindi hicho ushairi ulikuwa tayari
umesheheni ukwasi mkubwa wa lugha, na kama ulikuwa kweli umesheheni huu ukwasi
wa lugha alipaswa kutuonesha huo utajiri wa lugha anaouzungumzia katika
ushairi.
Senkoro (1988) anasema
kuwa ushairi uliibuka pale lugha ilipoanza katika kipindi cha uhayawani
(kipindi ambacho mwanadamu alipoanza kupambana na mazingira yake) kwenda katika
kipindi cha urazini (maana) ili kumwezesha binadamu na mazingira yake kwa
mfano, zana za kazi zilizotumika ziliwafanya waimbe kwa kufuata mdundo wa zana
hizo.
Masamba anasema
kwamba kimsingi chimbuko la ushairi wa Kiswahili ni waswahili wenyewe katika
nyimbo, ngoma nk ambazo ziliimbwa katika masuala ya kilimo, jando na unyago
n.k. Massamba anaendelea kusema kwamba nyimbo hizi zilikuwa zikiimbwa bila
kufuata vina na mizani lakini kwa kadri muda ulivyoenda walizidi kuziendeleza
na kuziboresha. Hivyo suala
la vina na mizani lililetwa na wageni sio kiini cha ushairi wa Kiswahili.
Mulokozi fasili
ya fasihi haiwezi kutenganishwa na utamaduni wa maisha ya watu. Anaelezea kuwa
ushairi wa Kiswahili hutumia lugha ya Kiswahili, hivyo ili kujua chimbuko la
ushairi wa Kiswahili ni lazima ujue juu ya waswahili wenyewe.
Udhaifu wa nadharia
Pamoja na kuwa
nadharia hii imeonesha kukubalika na wataalamu mbalimbali kama vile Senkoro,
Mayoka na Shekhe Amri Abeid, lakini bado ina mapungufu. Hii ni kwa sababu
imeshindwa kuonesha muda maalumu ambapo ushairi wa Kiswahili ulianza na ni wapi
ulianza kutumika. Hili ni suala ambalo linaumiza vichwa vya wataalamu
mbalimbali hadi hivi sasa, kwani hakuna mtaalamu yoyote aliyefanikiwa kuonesha
ni wapi na ni lini ushairi wa Kiswahili ulianza.
Hivyo basi,
kutokana na nadharia hizo mbili tunaungana na nadharia inayosema kuwa, chimbuko
la ushairi wa Kiswahili ni zao la waswahili wenyewe, kwa sababu waswahili wana
utamaduni wao ambao ulikuwepo kabla ya ujio wa Waarabu. Na waliutumia ushairi
huo katika shughuli mbalimbali za kijamii, kwa mfano katika harusi, jando na
unyago.
MAREJEO
Maoni
Chapisha Maoni