UCHAMBUZI WA RIWAYA ZA “NAGONA” NA
“MZINGILE”
1.0 Utangulizi
Katika makala haya
tutachambua riwaya za ‘Nagona’ na ‘Mzingile’. Katika kuchambua riwaya hizi
tutajikita katika kuangalia baadhi ya vipengele kama dhamira, falsafa, lugha,
mtindo wa usimulizi, wahusika, motifu na suala la ontolojia.
2.0 Maelezo kuhusu mwandishi na riwaya zake
2.1 Maelezo kuhusu mwandishi
Euphrase Kezilahabi alizaliwa mwaka 1944 katika
kijiji cha Namagondo kilichoko kisiwani Ukerewe katika ziwa Victoria nchini
Tanzania. Alipata elimu ya msingi huko kijijini Ukerewe na baadaye alijiunga na
seminari ndogo ya Nyegezi kwa ajili ya masomo ya upili. Baada ya kumaliza
alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es salaam mnamo mwaka 1967. Katika masomo yake
alijishughulisha na nadharia mbalimbali zihusuzo falsafa (Wamitila 1991:64).
Mnamo mwaka 1976 alitunukiwa shahada ya umahiri ya Chuo Kikuu cha Dar es
salaam, kabla ya kutunukiwa shahada nyingine ya umahiri ya Chuo Kikuu cha
Wisconsin-Madison mwaka 1982. Mwaka 1985, Kezilahabi alitunukiwa shahada ya
uzamivu katika fasihi na Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison huko Marekani baada
ya kukamilisha tasnifu yake ambayo ilihusu “African philosophy and the
problem of literature interpretation”. Baada ya masomo yake huko Marekani
alirudi kufundisha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam kabla ya
kuhamia Chuo Kikuu cha Botswana ambako anafundisha Lugha za Kiafrika na Fasihi.
Kezilahabi ameandika riwaya kadhaa kama vile
‘Nagona’, ‘Mzingile’, ‘Dunia Uwanja wa Fujo’, ‘Kichwa Maji’, ‘Gamba la Nyoka’.
Kezilahabi ameandika vitabu kadhaa vya ushairi ambavyo ni pamoja na ‘Karibu
Ndani’, ‘Kichomi’ na ‘Dhifa’. Katika medani ya tamthilia, msanii huyu amentunga
kazi tamthilia ya ‘Kaptula la Marx’ na
hadithi fupi kama vile ‘Mayai Waziri wa Maradhi’, ‘Cha Mnyonge Utakitapika
Hadharani’ nakadhalika.
Katika maisha yake Kezilahabi ametunukiwa tuzo
kadhaa kutokana na uandishi wake. Miongoni mwa tuzo hizo ni ile ya kumbukumbu
ya Edoardo Sanguinetti (1990) na ile ya kumbukumbu ya Shaaban Robert (1995)
(Mezger 2002: 76).
2.2 Maelezo kuhusu riwaya
zenyewe na muktadha wa utunzi
2.2.1 Riwaya ya Nagona
Riwaya hii ilichapishwa mwaka 1990. Riwaya hii
inahusu motifu ya safari ya nguli wa kiume amabaye jina lake halikubainishwa na
mwandishi. Nguli huyu anatumia muda mrefu kusafiri katika nyika na amechorwa
kwa kupatilizwa tajiriba na uwezo usio wa kawaida. Katika safari yake anakutana
na wanafalsafa mashuhuri. Miongoni mwao ni Marx, Nietzche na Freud ambao
wamekaa katika duara wakizungumza na roho zao ambazo wamezitema katika viganja
vyao. Kisha nguli huyu anagundua kuhusu kuwepo kwa paa wa ajabu na anaamua
kumfuatilia kwa kuangalia nyayo zake. Ili kumkamata anapaswa kuhimili mafumbo
mazito ya kimaisha ambayo yanaonekana kutokuwa na suluhu.
Ingawa majukumu hayo yanaonekana kuwa magumu, nguli
huyo anafanikiwa kumpata paa kwa kusaidiwa na wazee wanne ambao wana uwezo wa
ajabu. Baada ya kumpata paa ambaye anaonekana kuwa ni mwanamke mzuri, nguli
anashindwa kutimiza masharti ya kummilika paa na hatimaye anamtoroka.
Katika sura ya nane kuna maungamo yanaonekana
kufanyika ambayo kwa hakika ni vigumu kueleweka kama
yanafanywa na nguli au vinginevyo. Mhusika anaonekana kuungama dhambi za karne
mbili zilizopita ambazo wanadamu wamezitenda, anaungama dhambi hizo kwa padiri.
Kisha katika riwaya hii mnaonekana kuna ‘ngoma ya ungamo kuu’ inasubiriwa.
Ngoma inapowadia, makundi mbalimbali kama vile
ya wanafalsafa, wanasaikolojia, wanamapinduzi na vichaa yanajitokeza
kushindana. Nguli wa riwaya hii anashiriki ngoma hii akiwa na kundi la vichaa.
Mwisho wa riwaya hii msichana aitwaye ‘Nagona’ anazaliwa na nguli anamfuata.
2.2.2 Riwaya ya Mzingile
Riwaya hii inaanza na kisasili cha kuzaliwa
mtoto-kizee ambaye wanamwita Kakulu. Riwaya hii ni muendelezo wa riwaya ya
‘Nagona’. Kama ilivyo ‘Nagona’, riwaya hii nayo inahusu motifu ya safari ya
shujaa asiye na jina. Shujaa huyu anajiita ‘Mimi’ na ndiye msimulizi wa riwaya
hii. Huyu ‘Mimi’ anatumwa kupeleka ujumbe wa kifo cha Mkombozi wa pili kwa
babaye anayeitwa ‘Mzee’. Lakini safari yake ya kumtamfuta ‘Mzee’ inampeleka pia
katika kutafuta kiini na maana ya maisha. Mimi anafanikiwa kumpata Mzee katika
kijumba chake juu ya mlimani na kufanya naye mazungumzo. Hata hivyo Mimi
anashindwa kumshawishi Mzee kuhudhuria mazishi ya mwanaye. Kutokana na hali hii
Mimi anaamua kurudi na safari yake inampeleka katika kutafuta majibu ya maswali
ambayo hajaulizwa. Inamchukua Mimi karne nyingi kufika kijijini kwake.
Anapofika anagundua kuwa kijiji kimeharibiwa na mabomu ya nyuklia na kubaki
magofu.
Anapoingia katika nyumba yake iliyoharibiwa, Mimi
anamkuta Mzee na mazungumzo yanaendelea. Baada ya kitambo kirefu mvua inaanza
kunyesha na uoto unarudi katika hali yake. Katika kipindi hiki ‘mwanamke’
anajitokeza kimaajabu na kumuongoza ‘Mimi’ kuelekea ulimwengu mpya na kumuacha
‘Mzee’ ambaye baadaye anatoweka. ‘Mimi’ na ‘Mwanamke’ wanaishi pamoja na
kuanzisha ulimwengu mpya. Wote wanaonekana kujua makosa yaliyofanyika zamani.
Ili kuepukana na makosa hayo hapo baadaye, wanaamua kujenga ulimwengu mpya bila
kutumia maarifa yaliyopo.
2.2.3 Kuhusu utunzi wa
Kezilahabi
Kezilahabi alitunga Nagona (1990) na Mzingile
(1991), yaani, mwanzoni mwa miaka ya 90. Kipindi cha utunzi wa riwaya hizi
kufanana na kuingiliana kwake kunawafanya baadhi ya wanazuoni kuziita kazi hizi
RIWAYA KURWANA DOTO. Riwaya hizi zilitungwa miaka michache baada ya kutingwa
kwa diwani ya Karibu Ndani (1988). Maoni yetu ni kwamba diwani hii inahusiana
mno na riwaya hizi mbili. Uhusiano huu ni wa lugha na maudhui. Kwa jumla
tunaweza kusema kwamba sifa ya uandishi wa Kezilahabi ni matumizi ya lugha ya
mkato, yaani maneno yanapata uzito mkubwa na karibu kila neno ni taswira ama
sitiari. Zaidi lugha anayotumia ni lugha ya picha. Kwa hiyo, lugha ya picha
imepata uzito mkubwa katika kazi zake za kishairi na za riwaya kuliko kazi
zingine. Sitiari na wahusika wanafanana katika kazi zake tatu na pia falsafa inafanana.
Falsafa yake ni falsafa ya ontolojia
ambayo inachanganya falsafa ya kuwako ya Heidegger na falsafa ya ubuntu (utu)
ya Afrika. Umbo la riwaya za Nagona na Mzingile kifalsafa linachipukia katika
diwani ‘Karibu Ndani’ na inakua na kupata sehemu ya metafizikia. Metafizikia ni
falsafa ambayo inashughulikia kina cha kuwa
kwa dunia tofauti na ontolojia inayoshughulikia kuwapo kwa dunia. Tunathubutu kusema pia kuwa, tabia hii ya
kuendeleza mtazamo ina msingi wake katika kazi ya awali ya msanii huyu, yaani,
riwaya ya Rosa Mistika. Ukichunguza mjengo na mbinu za uwasilishaji wa
vipengele mbalimbali vya kifani na maudhui katika riwaya yake ya Dunia Uwanja
wa Fujo utakubali kuwa kuna kitu ambacho msanii huyu kinamtatiza na jibu la
fumbo bado hajalipata.
Kwa kutumia nadharia ya
Umuundo Mpya ambayo iatafafnuliwa hapo baadaye, bila shaka yoyote tunaona dhana
ya maisha kwa msanii huyu, ni kitu ambacho hakina maana yoyote. Tunatumia
dondoo inayopatikana katika riwaya yake ya Dunia Uwanja wa Fujo kushikilia
msimamo wetu huu. Ni muhimu kuangalia diwani ya ‘Karibu Ndani’ kwa sababu
katika diwani hii tunapata chimbuko na sababu ya safari ambayo ni muundo wa
riwaya za ‘Nagona’ na ‘Mzingile’. Kwa mfano katika shairi la ‘Safari’ mistari
ya mwisho tunasoma:
Wakati nisafiripo kwenda mawioni usiku
nitazichuma karanga zote zing’aazo angani
na kuziweka ndani ya mifuko ya suruali
langu:
kisha nitazila moja moja toka mifuko iliyotuna.
Nitakapofika nitafungua kinywa kwa chapati
ya dhahabu kabla haijapoa kilimani;
halafu hapatakuwa na mwaga tena,
kwani taswira na sitiari zote za nuru
hazikutufikisha pasipo giza.
Kwa hiyo nasi kama mkulima kipofu
nitapanda mbegu gizani.
Hapa taswira na
sitiari za aina hizi ni sitiari chakavu na mshairi amekuwa mkulima kipofu ili
azae sitiari zenye uhai. Zaidi kama tunavyosoma shairi la ‘Hii Moja Hadithi’
katika diwani hiyo tunapata kwamba kazi hizi tatu, yaani ‘Nagona’, ‘Mzingile’
na ‘Karibu Ndani’ zina sifa zinazofanana.
Hii moja hadithi
Na hii moja hadithi kuwasimulia watoto,
ya mtu aliyesita alipofika njia panda,
akaongozwa ile njia na ndege akirukaruka:
ujana wangu ulianza kwenye ua waridi fumbo,
ukaishia kwenye gamba kandokando ya mto,
baada ya kisu kutokata kamba nilioning’inia.
Nimepanda vilima na kushuka hadi pangoni,
nikaselea magofuni karibu na kisima cha
uzima.
Nimejifunza lugha nyingi za vichaa na
wanyama,
nimeuona ule mji wenye lugha ya kimya,
nao huo mto wa damu ilimopotea miswada.
Nimeshuhudia pia utapikaji wa roho,
na jinsi zilivyopotea kwenye maji ya uzima.
Nimeicheza usiku kucha ngoma ya vurumai.
Baada ya haya yote jua likapatwa
nikaelekea kitanda cha mtoto alipolala
Nagona
au pale kilimani watoto walipoketi
hii moja hadithi watoto wataipenda.
Hiyo
inatuonyesha kwamba kezilahabi alitaka kupita mipaka kati ya ushairi na
nathari.
3.0 Fani na Maudhui ya riwaya hizi
3.1 Maudhui
Katika sehemu hii tutajikita katika
kuchambua baadhi ya vipengele vya maudhui kama vile dhamira zinazojitokeza
katika riwaya hizi na falsafa ya mwandishi wa riwaya hizi. Katika kuchambua
dhamira tutaanza kufafanua dhamira zinazojitokeza katika riwaya ya ‘Nagona’ na
kisha tutafafanua dhamira zinazojitokeza katika riwaya ya ‘Mzingile’. Hivyo
zifuatazo ni baadhi ya dhamira zinazojitokeza katika riwaya ya ‘Nagona’:
(i) Suala la falsafa
Mwandishi wa
riwaya hii anashughulishwa na kusaili mawazo ya wanafalsafa mbalimbali wa
ulimwengu hususani wanafalsafa wa kimagharibi. Katika ‘Nagona’ mwandishi
anatuonyesha Socrates, Aristotle, Hegel, Nietzsche, Marx na Freud wakiwa katika
duara ambalo ni ishara ya ukamilifu wa maisha. Wanafalsafa hawa wanaonyeshwa
wakiwa wamezitapika roho zao na kuzungumza nazo ili kuzitakasa (Sura ya 3 uk.
15). Hata hivyo wanashindwa kuzisafisha roho zao baada ya kupitiwa na mkondo wa
mto na wanafukuzwa.
Katika suala
hili Kezilahabi anatuonyesha kuwa ingawa askari hawa wa mwanga wametumia muda
mwingi katika maisha yao kuusaka ukweli bado hawakuweza kuupata. Diegner (2005:29)
anasema ‘kushindwa kwa wanafalsafa hawa kuna maana mbili: mosi, ni kuutaka
ulimwengu kutazama na kutathmini upya mchango wa wanafalsafa hao; pili ni
kuonyesha ukomo wa falsafa kama njia ya kuusaka ukweli, kama njia ya kusafisha
roho zetu, ambayo ina maana ya kuwa viumbe bora zaidi’.
(ii) Suala la dini
Riwaya hii licha
ya kuhakiki mawazo ya wanafalsafa mbalimbali pia inahakiki suala la dini. Jambo
hili pia linajitokeza katika riwaya ya ‘Mzingile’. Katika sura ya kwanza
tunamuona nguli wa riwaya hii anatazama maiti ambayo katika mkono mmoja
amepakatishwa Biblia Takatifu na mkono mwingine Korani Tukufu (uk. 2-3). Kwa
maoni yetu, katika riwaya hii kwa kiasi kikubwa Kezilahabi anajishughulisha
zaidi na viongozi wa dini na si dini yenyewe. Kwa mfano (katika sura ya 1
ukurasa 4-6) Kezilahabi anamchora padre kama mlevi asiyeweza kuwa na dira na
pia padre anachorwa kama mtu asiyeweza kutoa majibu ya masuala muhimu yahusuyo
maisha. Pamoja na hayo, inaonekana Kezilahabi anatambua mchango wa dini katika
kumuongoza mwanadamu katika harakati za kutafuta kiini na maana ya maisha.
Zaidi ya hayo,
kwa maoni yetu katika riwaya hii maungamo yanasawiriwa kama kipengele muhimu
katika kujenga utu. Suala hili linajidhihirisha zaidi katika sura ya 8 ambayo
inaongelea zaidi maungamo ya dhambi zote za wanadamu.
(iii) Tafakuri kama njia ya kuufikia ukweli
Katika riwaya
hii mwandishi anasisitiza zaidi katika tafakuri ili kuufikia ukweli. Umuhimu wa
kufikiri katika kuufikia ukweli unajidhihirisha katika kutatua fumbo la
‘Nagona’ ni nini. Katika ukurasa wa 44 anaonekana kuzungumza na babu yake kama
ifuatavyo:
“Lakini babu, huyu Nagona ni
nani?”
“Utamwona, na utakapomwona
utashangaa kwa nini ulikuwa humwoni
Maana daima yu karibu nawe.
Muhimu ni kufikiri, utashi na nia”.
Katika
mazungumzo hayo kinachoonekana ni Kezilahabi kusisitiza watu kufanya tafakuri.
Anatumia ‘Nagona’ kama fumbo ambalo ili kulifumbua tunahitaji kufanya tafakuri.
Hivyo jambo muhimu katika kuusaka ukweli ni kufikiri, utashi na nia kama
asemavyo Kezilahabi kupitia wahusika wake.
(iv) Umuhimu wa wazee
Riwaya hii licha
ya kujikita katika kushughulikia masuala ya kifalsafa, imewapa umuhimu mkubwa
wazee. Riwaya hii inatuonyesha kuwa wazee wana hazina kubwa ya maarifa ambayo
hatuna budi kujifunza kutoka kwao. Katika riwaya hii tunamuona nguli hapa na
pale akipata msaada na ushauri wa wazee katika safari yake ya kumsaka paa.
Katika sura ya 2 ya riwaya hii Kezilahabi anamchora babu yake na nguli kuwa ni
mtu mwenye maarifa mengi, maarifa ambayo yanampatia nguli mwanga wa kumsaka paa.
Katika ukurasa wa 9 Kezilahabi anaandika:
“Babu yangu alijulikana sana kijijini. Wazee
wengi walifika kutafuta
mawaidha kuhusu migogoro yao,
wengine walifika tu kusikiliza heki-
ma yake na masimulizi ya
historia ya wakati uliopita. Mara nyingi ni-
likaa karibu naye kusikiliza
maongezi yake na wazee, ingawa hapaku-
wa mahali pangu. Utamsikia
akiniambia katikati ya mazungumzo:
‘Bwana mdogo! Nakutaka unisikilize
vizuri. Nataka uwe shahidi wa
kweli. Ishara itakapotokea
uifuate hadi kwenye kitovu cha duara”.
Maelezo hayo
kutoka katika riwaya yanaonyesha jinsi mzee anavyochukuliwa. Hapa mzee
anachukuliwa kama mtu mwenye maarifa na hekima. Jambo hili linathibitishwa na
methali isemayo ‘kuishi kwingi kuona mengi’.
Baada ya
kufafanua dhamira zinazojitokeza katika riwaya ya ‘Nagona’, katika sehemu
inayofuata tutafafanua dhamira zinazojitokeza katika riwaya ya ‘Mzingile’. Kwa
ufupi katika riwaya ya ‘Mzingile’ kuna dhamira zifuatazo:
(i) Suala la maana ya maisha
Katika riwaya
hii ya ‘Mzingile’ suala la maana ya maisha linapewa uzito mkubwa. Dhamira hii
imejengwa katika taswira ya safari, safari ya kutafuta kiini na maana ya
maisha. Safari hii inafanywa na nguli anayeamua kumsaka Mzee ili ahudhurie
mazishi ya mwanaye. Anapofanikiwa kumpata, Mzee anagoma na kudai kuwa hana
mtoto . Nguli anaamua kurudi na kukuta kijiji chake kimeteketea kwa sababu ya
mabomu ya nyuklia.
Kwa jumla safari
ya nguli kumtafuta Mzee ni juhudi za wanadamu katika kutafuta kiini cha maisha
yao na maisha ya viumbe wengine na maana ya maisha hayo. Riwaya hii inayatazama
maisha kama suala tata lisiloweza kutatulika. Wakati baadhi ya watu
wanajitahidi kufanya uvumbuzi ili kuboresha maisha ya wanadamu, wengine hujikita
katika kuvumbua silaha ambazo hutumika kuteketeza viumbe. Riwaya hii inakwenda
mbali zaidi kwa kuonyesha kuwa ingawa kuna mengi yamefanywa lakini maisha ya
wanadamu bado ni kizungumkuti kwa sababu dhiki bado inatawala.
(ii) Imani na mantiki
Dhamira hii
inajitokeza kwa kutazama mazungumzo ya Mzee na nguli wa riwaya hii katika
ukurasa wa 57. Katika ukurasa huo tunasoma:
“. . . Kila wakati unachanganya
kuwako kwako na kwangu; uhalisia wako
unauchanganya na wangu, na
kitambulisho chako unakifanya kuwa changu.
Si hivyo tu. Nimekusikia mara
nyingi ukichanganya kitambulisho cha baba
yako na changu. Na kama si cha
baba yako basi unarudi nyuma kwa babu na
babu hadi kunifikia mimi!
Tutasuluhisha lini jambo hili ili kila mmoja wetu
awe kama alivyo na mwenye uhuru
wake kamili?”
Haya ni maneno
ya Mzee akimuambia kijana. Akifafanua maelezo haya ya Mzee, Wamitila (1991:66)
anasema kuwa “yanatoa mwangwi wa kauli ya Soren Kierkegaard kuwa Mungu aliumba
hali ambayo yeye mwenyewe hatambuliwi na kwamba ni utu ndio utakaomtambua,
utakaomuona na kumzoea kupitia imani”. Hata hivyo kwa maoni yetu, Kezilahabi
anakwenda mbali zaidi ya imani kama njia pekee ya inayomuwezesha mwanadamu
kumzoea Mungu. Anaonyesha hatari ya kutegemea imani kama njia pekee ya kutatua
matatizo yanayotukabili. Hii ina maana kuwa, tunapaswa kutumia akili zetu
ingawa tuna imani katika kutatua matatizo yetu.
(iii) Suala la ujinga
Kezilahabi anatuonyesha
kuwa katika ulimwengu ujinga umekithiri na kwamba wanahitajika vichaa
watakaoleta mwanga ili kuusaidia ulimwengu usiteketee. Katika ukurasa wa 28
kuna wimbo ufuatao:
“Ninaimba juu ya giza
lililougubika ulimwengu
Tumetembea katika msitu wa kurasa
potovu
Na kutafuna kila neno na
kila aina ya wino,
Tumemeza yapashwayo
kunywewa,
Na kucheua yatakiwayo
kumezwa. . .”
Katika wimbo huu
Kezilahabi anatuonyesha jinsi ujinga ulivyokithiri. Anatueleza kuwa kwa sababu
ya ujinga tunafanya yale tusiyopaswa kuyafanya nay ale tunayopaswa kuyafanya
hatuyafanyi.
3.1.2 Falsafa
Kama
tulivyodokeza katika kipengele namba 2.2.3, falsafa ya Kezilahabi inayoonekana
katika riwaya za ‘Nagona’ na ‘Mzingile’ ni falsafa ya kuwako lakini ina sehemu
mpya ya metafizikia. Hayo ni matokeo ya kuchanganya suala la ‘kuwa’ (sehemu ya
metafizikia) na suala la ‘kuwako’ (sehemu ya ontolojia). Kuwako ni falsafa
inayotokana na falsafa ya Da-sein ya Heidegger. Falsafa ya kuwako ya Kezilahabi
inahusu maisha ya mtu mwenye dhiki na Afrika. Lakini mawazo yote ya falsafa hii
hayatokani na Heidegger tu bali pia na falsafa ya utu. Zaidi Kezilahabi
anafikiri kuhusu hali ya Waafrika, kama anavyosema M.M. Mulokozi (Diegner,
62:2002):
Msomi wa Kiafrika ni Kichwamaji. Amechanganyika
katika kichwa chake kwa sababu ya kupokea vitu vingi kutoka nje, imani, lugha,
mila na kadhalika. Ametekwa na mambo ya kigeni kwa kiasi kikubwa. Namna ya
kichaa. Ndiyo [Kezilahabi] anamwita Kichwamaji.
Katika ‘Nagona’ na ‘Mzingile’ falsafa hii
inachanganya alama na visasili vya Afrika kama ubuyu, wahusika, ngoma
nakadhalika. Ugumu wa kuelewa na kueleza falsafa hii unatokana na namna ilivyoandikwa
yaani falsafa yake yote inaelezwa kwa sitiari kama falsafa ya asili ya Afrika
na kuathiriwa na mawazo ya akina Plato, Nietzsche na wengineo. Kwa mfano,
ishara ya duara inatokana na falsafa ya asili ya Afrika kama sitiari ya maisha
na mwendo wa wakati, lakini pia inatokana na Ewiger Wiederkehr (rudiomilele tu)
ya falsafa ya Nietzsche. Rudiomilele katika falsafa ya Nietzsche ni rudio
ambalo linamwezesha mtu kuwa kamili na kuzaa daima. Mtu mpya tu anaweza
kukubali na kuishi katika wakati wa rudiomilele, hiki ni kizazi cha utu mpya.
Alama za duara na kuzaa zinabeba alama nyingine za ngoma ambazo ni topos katika
kazi hizi na pia katika kazi ya Nietzsche.
Kwa hiyo wote
wawili wanatumia ngoma kama chombo ambacho kinaweza kufungua mlango “uelekeao
katikati ya ujuzi na urazini mpya, mwanzo wa kizazi” kama anavyoandika Kezilahabi
katika shairi la ‘Kisima’. Ingawa wanatumia ngoma kama tendo lenye uwezo wa
kufungua mlango wa uzalishaji wanatueleza kwamba tendo kubwa la kuzaa linatokea
wakati wa kimya. Tusome ukurasa 77 (Nietzsche, 1882):
Matukio makuu
yanatukia wakati wa kimya.
Maneno haya
tunaweza kulinganisha na “Ngoma ya kimya” katika diwani ya Karibu Ndani ambamo kuna ukimya.
Muundo wa msingi wa riwaya hizi ni safari.
Topo hii inajirudia sana katika visasili vya Afrika. Kwa hiyo ni alama ya
riwaya ambayo inaonekana kutuambia kuhusu namna zilivyoandikwa riwaya hizi na
mwendo wa muhusika mkuu, mimi. Zaidi ni alama ya falsafa ya Nietzsche wakati
anazungumza kuhusu rudiomilele. Kwa mwanafalsafa wa Kijerumani mtu mpya ambaye
anaweza kukubaliana na rudiomilele ni mtu ambaye alisafiri kwa sababu alipoteza
nchi yake lakini pia nyumba yake na kila kitu.
3.2 Fani ya riwaya hizi
3.2.1 Mbinu ya Usimulizi
Katika kuandika
riwaya hizi Kezilahabi ametumia mbinu mbalimbali za usimulizi. Utumiaji wa
mbinu hizi unatokana na uchanganyaji wa nafsi katika kusumulia visa
vinavyojitokeza katika riwaya hii. Uchanganyaji huu wa nafsi katika usimulizi
unazifanya riwaya hizi kuwa riwaya zinazofuata mkondo wa usasa na ubada-usasa.
Kwa kiasi kikubwa katika riwaya hizi Kezilahabi ametumia nafsi ya kwanza umoja,
ambapo kiwakilishi ‘mimi’ kimetumika. Nafsi hii imejitokeza katika riwaya zote
mbili ili kumfanya msomaji aingie ndani ya ulimwengu wa mwandishi. Kwa mfano
katika ‘Mzingile’(uk.11) tunasoma ‘niliporudi alipandisha kidogo utambi wa taa
. . .’ Katika sentensi hii kiambishi ‘ni’ kinarejelea nafsi ya kwanza umoja.
Pia katika ‘Nagona’ (uk. 1) tunasoma, ‘niliweza bado kuona msitu mkubwa nyuma
yangu . . .’ Matumizi ya nafsi hii yanamfanya msimulizi kuwa mhusika kama
ilivyo katika riwaya hizi.
Pia kuna
matumizi ya nafsi ya pili katika riwaya hizi. Katika riwaya hizi nafsi hii
imetumika kila mhusika mkuu anapoonekana akifahamishwa jambo fulani. Kwa mfano
katika ‘Nagona’ tunasoma ‘unauona mti ule . . .’ Zaidi mwandishi ametumia nafsi
ya tatu ili kumuwezesha kusimulia alichoona na wanachokifikiria wahusika wake.
3.2.2 Lugha
Lugha katika riwaya hizi ina uzito wa sitiari
na karibu kila neno ni taswira, sitiari au alama. Lugha hii inaonekana kuwa
karibu na lugha ya kishairi kuliko lugha ya kinathari. Kwa jumla riwaya hizi
zimetumia lugha ya kiwango cha juu ambacho si rahisi kuielewa bila tafakuri ya
kina. Kuna matumizi makubwa ya jazanda hali inayofanya riwaya hizi kuwa pevu.
Miongoni mwa ishara zilizotumika ni mbuyu ambao unaashiria imani za kidini na
kafara; mzee inaashiria busara na uungu. Pia kuna matumizi ya lugha ya picha.
Kwa mfano katika riwaya zote kuna taswira ya safari ya mhusika mkuu ambayo
inayorejelea jitihada za mwanadamu katika kuusaka ukweli, kiini na maana ya
maisha.
3.2.2.1 Tamathali za semi
Katika riwaya
hizi kumetumika tamathali mbalimbali za semi ili kumathilisha jambo kwa
kulifananisha na jingine. Tamathali zilizotumika katika riwaya hizi ni pamoja
na tashibiha, sitiari, n. k.
3.2.2.1.1 Tashibiha
Hii ni tamathali
ambayo inalinganisha vitu viwili kwa kutumia viunganishi kama vile: mithili ya,
kama, sawa sawa na, n.k. Katika riwaya hizi kuna tashibiha zifuatazo:
·
“Alichezeshachezesha masikio yake kama ng’ombe”
(Mzingile uk. 11). Tamathali hii inalinganisha tukio la mzee kuchezesha masikio
yake na ng’ombe achezeshavyo masikio yake. Tamathali hii imetumika ili
kuonyesha utayari wa mzee katika kusikiliza ujumbe aliopelekewa.
·
“Maisha ni kama mkufu” (Mzingile uk. 6).
Tamathali hii inalinganisha maisha na mkufu ili kuonyesha kuwa ili maisha
yakamilike tunahitaji kufanya juhudi katika kutafuta, ni kama uundaji wa mkufu
unaohitaji kuunganisha vipande.
·
“Sote tulikuwa tumeinama vichwa chini kama
walinzi wanaosujudu mfalme apitae” (Nagona uk. 46). Tamathali hii inalinganisha
tendo la kuinamisha vichwa na kusujudu. Tamathali hii imejitokeza kuelezea hali
ya huzuni baada ya babu kufariki. Ni ishara ya kutafakari maana ya maisha kwa
binadamu.
·
“Kumbikumbi wakawa kama sayari mpya ambazo ndio
kwanza zimegunduliwa” (Nagona uk. 46). Hii imetumika kujenga taswira ya ufuasi
kwamba baada ya kifo cha babu kulijitokeza wafuasi wa mawazo yake.
3.2.2.1.2 Sitiari
Hii ni tamathali
ya semi inayolinganisha vitu bila kutmia viunganishi. Tamathali hii hutumika
kiishara na kitaswira. Zifuatazo ni baadhi ya sitiari zinazojitokeza katika
riwaya hizi:
- “Maisha kitu cha ajabu” (Nagona uk. 43). Tamathali hii imetumika kueleza utata katika kufumbua fumbo la maisha ni nini. Hapa maisha yanatazamwa kama kitu kisichoeleweka.
- “Ulimwengu tambara bovu” (Nagona uk. 24). Sitiari hii inalinganisha ulimwengu na tambara bovu. Katika muktadha huu imetumika kueleza kuwa ulimwengu si kitu cha kutegemea ni kama tambara bovu ambalo muda wowote linaweza kuchanika.
- “Maisha yenyewe ni mzaha mkubwa . . .” (Mzingile uk. 13). Hapa maisha yanalinganishwa na mzaha ili kuonyesha kuwa maisha ni kama vurumai.
3.2.2.2 Methali
Katika riwaya
hii pia kumetumika methali kadhaa ili kujenga mazingira ya kiutamaduni na
kusisitiza jambo. Miongoni mwa methali zilizotumika katika riwaya hizi ni hizi
zifuatazo:
- “Kipya kinyemi ingawa kidonda” (Mzingile uk. 37). Methali hii imejitokeza wakati wanawake kadhaa wamepelekwa kuonyesha maumbile yao, wanawake hao waliwakuta wenzao ambao walikuwepo tangu zamani. Methali hii imetumika kuonyesha umuhimu wa watu kuthamini mambo yao.
- “Asiyesikia la mkuu huvunjika guu” (Mzingile uk. 1). Methali hii aliitamka Kakulu ili kuonyesha kuwa ulimwengu unaangamia kwa kudharau ushauri wa wahenga. Pia imetumika kuuonya ulimwengu.
3.2.2.3 Misemo
Katika riwaya
hizi kumetumika misemo kadhaa na kuifanya lugha iliyotumika katika riwaya hizi
kuwa ni ya kufikirisha zaidi. Miongoni mwa misemo hiyo ni hii ifuatayo:
- “Mkubwa haibi anachukua” (Mzingile uk. 45). Msemo huu umetumika ili kuonyesha utetezi wanaoufanya viongozi walio madarakani katika kuhalalisha uporaji wa mali ya umma.
- “. . .usimwamini mwanamke mzuri, na mbaya mwambae” (Mzingile uk. 41). Msemo huu unajitokeza baada ya mwanamke kutoka bara la Afrika kukataa kuuudhalilisha utu wake. Msemo huu umetumika kuonyesha umuhimu wa kuwa na tahadhari katika kufanya mambo.
- “Wakati titi la nyati, hukamuliwa kwa shaka” (Nagona uk. 44). Msemo huu umetokana na mshororo wa shairi, na katika riwaya hii umetumika kuonyesha umuhimu wa kutumia wakati kwa tahadhari.
Kwa jumla riwaya
hizi zimetumia lugha ya kifalsafa huku mwandishi akitumia pia maneno kutoka
lugha za kigeni kama kiingerzeza, kilatini, na kiitaliano.
3.2.3 Wahusika
Wahusika wa
riwaya hizi wanasifiwa zaidi kwa ukosekano kuliko uelezo kamili kuhusu wao. Wao
wanasifiwa kama alama au sitiari ya safari kama motifu ya riwaya hizi. Tuanze
na muhusika mkuu, mimi. Mimi sio jina
la kipekee bali ni kiwakilishi cha nafsi ya kwanza umoja. Utumiaji wa kiwakilishi
mimi unampa Kezilahabi uwezo wa
kukuribisha ndani msomaji katika dunia yake. Safari ya mimi ni safari ya utu
kama safari ya ndani katika komedia ya dante ambayo anasafiri kwenye moto mpaka
mbinguni ili kusafisha utu. Utumiaji wa mimi unaonekana kuwa chombo cha ushairi
wa kihisia ambao msomaji akiusoma anaingia ghafla katika dunia ya shairi ambalo
mwandishi alitunga. Kwa wahusika wengine tumepata vikundi viwili ambavyo vinajitokeza
kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa riwaya hizi, yaani Nagona na Kakulu. Hapa Nagona
ni kama alama ya wanawake ambao wanajitokeza katika riwaya na Kakulu kama alama
ya wazee. Tueleze mahusiano haya kwenye mchoro ufuatao:
DUNIA INAYONYESHWA KWENYE RIWAYA ZA NAGONA NA
MZINGILE
4.0 Vipengele vingine vinavyojitokeza
katika riwaya hizi
4.1 Suala la motifu
Hiki ni
kipengele kimojawapo kinachojitokeza katika riwaya hizi. Motifu ni kipengele
cha kijadi au kikaida cha kifani au kimaudhui kinachojitokeza katika kazi za
kifasihi ili kutoa ujumbe fulani. Katika fasihi kuna motifu mbalimbali kama
vile safari, msako, mama wa kambo, Bi. Kizee, mnyonge anayemshinda mwenye
nguvu, n.k. Katika riwaya za ‘Nagona’ na ‘Mzingile’ kuna motifu zifuatazo:
4.1.1 Motifu ya safari
Hii ni motifu
ambayo imetawala katika riwaya hizi, na ndio msingi mkuu wa muundo wa riwaya
hizi. Riwaya zote mbili zimeandikwa kwa muundo wa kisafari ambapo wahusika wa
riwaya hizi wanaonekana wakiwa katika safari, safari ambayo ni taswira ya
juhudi za mwanadamu katika kuutafuta ukweli, maana na kiini cha maisha yake.
Kwa mfano katika ‘Nagona’ tunamuona muhusika ‘mimi’ akifunga safari kuelekea
kumtafuta paa ambaye ni mwanamke mzuri, ishara ya ukweli. Pia katika ‘Mzingile’
tunamuona muhusika ‘mimi’ akifunga safari kumsaka ‘mzee’ ambaye ni ishara ya
Mungu. Safari hii ya mimi ni sehemu ya juhudi ya mwanadamu kutaka kufahamu
kiini cha maisha yake.
4.1.2 Motifu ya msako
Hii ni motifu
nyingine ambayo imejitokeza katika riwaya hizi. Katika riwaya zote tunamwona
muhusika mkuu akiwa katika safari lakini safari yenyewe ni katika kusaka kitu
au jambo fulani. Kwa mfano katika ‘Nagona’ tunamwona ‘mimi’ akiwa anamsaka paa
ambaye anaashiria ukweli na maarifa wakati katika ‘Mzingile’ tunamwona ‘mimi’
akiwa anamsaka ‘mzee’ ili ashiriki mazishi ya mwanae. Msako huu unaofanywa na
‘mimi’ katika ‘Mzingile’ ni msako wa maana na kiini cha maisha.
4.2 Suala la ontolojia
Hiki ni
kipengele kingine kinachojidhirisha katika riwaya hizi. Zaidi ya kushughulishwa
na masuala tuliyoyaeleza, mwandishi pia ameshughulikia suala la mtazamo wa
jamii kuhusu maisha na uwapo wa mwanadamu na ulimwengu kwa jumla. Katika
kushughulikia suala hili mwandishi ameonyesha mtazamo wa Wabantu kuhusu asili
ya maisha na ulimwengu pamoja na uwapo wao. Zifuatazo ni baadhi ya dhana za
ontolojia ya kibantu zinazojitokeza katika riwaya hizi:
4.2.1 Dhana ya wakati
Dhana ya wakati
kwa Wabantu ni wakati ulio katika duara. Kwa Wabantu wakati ni duara tofauti na
jamii nyingine. Dhana ya wakati katika duara ni dhana ya wakati usiokwisha,
wakati uso-kikomo, unaojirudia. Katika riwaya hizi dhana hii ya wakati katika
duara inajidhihirisha katika riwaya hizi kwa kuingalia safari ya muhusika mimi
ambaye anaanza safari yake kutoka sehemu A kupitia B hadi C na kisha kurejea
mwanzo wa safari yake, yaani sehemu A.
4.2.2 Dhana ya uzazi
Katika mtazamo
wa Wabantu uzazi unachukuliwa kuwa ndio njia pekee ya ‘uzima wa milele’ na
kwamba ugumba ni laana. Kwa Wabantu uzazi ndio njia pekee inayowahakikishia
wanadamu kuendelea kuishi. Katika riwaya ya ‘Nagona’ suala hili
linajidhihirisha ukurasa wa 62 ambapo mwanamke aliye na ujauzito anajifungua.
Pia katika riwaya ya ‘Mzingile’ suala la uzazi linaonekana katika kisasili cha
Kakulu ambapo mwanamke anajifungua mtoto ambaye watu wanamwita Kakulu.
4.2.3 Dhana ya kuheshimu wahenga
Katika riwaya
hizi suala la heshima kwa wahenga linajitokeza. Katika mtazamo wa Wabantu
heshima kwa wahenga inajidhirisha katika kufanya matambiko ili kuhakikisha
uwapo wao. Suala hili linajidhihirisha zaidi kwa kuangalia kisasili cha Kakulu
ambaye baada ya kufa watu wa kijiji alichoishi wanaamua kuanza kufanya
matambiko katika mbuyu ili kumkumbuka.
4.2.3 Dhana ya mtu kuweza kubadilisha jaala
yake
Katika riwaya
hizi Wabantu wanaonyeshwa kuwa wanaamini katika uwezo wa mtu binafsi katika
kubadilisha au kuongoza jaala yake. Huu ndio mtazamo wa Wabantu. Suala hili
linajidhihirisha kwa kumuangalia muhusika ‘mimi’ ambaye anafunga safari ili
kusaka jaala yake mwenyewe.
5.0 Hitimisho
Kwa jumla riwaya
hizi ni riwaya pacha ambazo zina muundo wa kisafari. Riwaya hizi zinasawiri
masuala mbalimbali ya kijamii na kifalsafa na ni riwaya zilizo katika mkondo wa
usasa na ubada-usasa kwani zaidi ya kutetea dunia dhidi ya maangamizi ya
mataifa makubwa pia zinajikita katika kuangalia matatizo ya dunia ya tatu.
Riwaya hizi zinahusiana na kukamilishana. Uhusiano wa riwaya hizi unatokana na
kuhusisha visasili vya Kiafrika, matumizi ya sentensi fupifupi zenye
kufikirisha, matumizi ya wahusika wa ukosekano kuliko maelwzo kamili, na ufupi
wa riwaya zenyewe lakini zenye uchangamani mkubwa.
MAREJEO
Diegner, L.
(2005) Intertextuality in the
Contemporary Swahili Novel:
Euphrase
Kezilahabi’s Nagona and William E. Mkufya’s Ziraili na Zirani. Kiswahili
Forum 12 (uk. 25-35).
Gromov, M. D.
(1998) Nagona and Mzingile: Novel,Tale or
Parable? AAP55 (uk.73-78)
Kezilahabi, E.
(1990) Nagona. Dar es salaam, Dar es
salaam University Press.
…………… (1991) Mzingile.
Dar es salaam, Dar es salaam University Press.
Wamitila, K. W.
(1991) Nagona and Mzingile:
Kezilahabi’s Metaphysics.
Kiswahili:
Jarida la Taasisi ya Uchunguzi
wa Kiswahili Juz. 58.
………………. (1997) Contemptus Mundi and Carpe Diem Motifs in Kezilahabi’s
Works. Kiswahili:
Jarida la Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili Juz. 60.
Maoni
Chapisha Maoni