1.0 Utangulizi
Kazi
hii inahusu uchambuzi wa fani na maudhui katika riwaya ya “Adili na Nduguze” iliyoandikwa na Shaban Robert mwaka
1952. Katika kujadili riwaya hii tutaeleza dhana ya riwaya, usuli wa mwandishi,
muhtasari wa kitabu chenyewe, nadharia zitakazotumika kuchambua fani na maudhui
ya kitabu hiki, uchambuzi wa fani na maudhui na hitimisho.
1.1 Dhana ya Riwaya
Kwa mujibu wa Madumulla (2009)
akimrejelea Msokile (1992) anafafanua kuwa riwaya ni kazi ya sanaa ya kubuni,
ni maandishi ya nathari (ujazo) yanayosimulia hadithi ambayo kwa kawaida ina
uzito, upana, urefu wa kutosha, ina wahusika wengi wenye tabia mbalimbali, ina
migogoro mingi mikubwa na midogo.
Senkoro (1982) anasema riwaya ni
hadithi ndefu ya kubuni yenye visa vingi, wahusika zaidi ya mmoja, na yenye
mazungumzo na maelezo yanayozingatia kwa undani na upana maisha ya jamii.
Wamitila (2003), Samwel na wenzake
(2013), wanasema kuwa riwaya ni kazi andishi ya fasihi ambayo kwa kawaida ni
ndefu zaidi kuliko hadithi fupi. Urefu wa riwaya maana yake ni kwamba msuko
simulizi umejengeka vizuri, kuna wahusika wengi, inaenea muda mrefu, na mada
zake ni nzito na pana kiasi. Mifano mizuri ya riwaya kwa lugha ya Kiswahili ni
“Nagona” au “Mzingile” riwaya za mwandishi Euphrase Kezilahabi.
Kwa ujumla riwaya ni hadithi ndefu
za kubuni zenye wahusika wengi au wachache zinazoelezea maisha ya mtu au jamii
fulani.
1.2 Usuli wa Mwandishi
Sheikh Shaaban Bin Robert alizaliwa tarehe mosi January mwaka wa
1901 katika kijiji cha Vibambani, mahali paitwapo Machui, maili sita kusini ya
Tanga. Yakisiwa kuwa jina hili la 'Robert' lilitokana na matamshi mabaya ya
Jina lake alilopewa akiwa skuli, Msimbazi, kwa kuwa baba yake hakuitwa Robert.
Mara nyingi aliandika jina lake kama "Roberts"
Baba yake alifanya kazi kama karani katika Shamba la makonge la Amboni. Mama yake alikuwa Mdigo. Yasemekana kuwa wazazi hawa wawili walikuwa wa ukoo wa Mganga wa kabila la Kiyao. Lakini, Sheikh Shaaban alikataa kuitwa Myao akawa mmoja wa watu wachache waliojiita Waswahili.
Baba yake alifanya kazi kama karani katika Shamba la makonge la Amboni. Mama yake alikuwa Mdigo. Yasemekana kuwa wazazi hawa wawili walikuwa wa ukoo wa Mganga wa kabila la Kiyao. Lakini, Sheikh Shaaban alikataa kuitwa Myao akawa mmoja wa watu wachache waliojiita Waswahili.
Shaaban alitafuta mke wake wa
kwanza kwa utulivu na makini kwa miaka kumi. Alitaka mke mzuri, mwaminifu na
mwenye tabia ya kuigwa katika nyumba. Alifanikiwa hata akaoa mke wake Amina.
Baada ya miaka kumi mke wake alifariki dunia. Shaabani aliomboleza kifo cha mke
wake hata akatunga shairi la msiba huo. Yasemekana kuwa mke wake aliacha watoto
watano, dada yake mwana Saumu na mama yake. Alivumilia maisha ya ugane kwa
miaka mitano. Kisha akaposa mke wake wa pili na kuoa tena. Alioa mara tatu.
Kuanzia mwaka wa 1926 hata1944, Shaaban alifanya kazi na Idara ya Forodha, Pangani. Alikuwa mtu mwenye kufanya kazi yake kwa uangalifu na uvumilivu hata alipandishwa vyeo viwili katika kazi hii: "Grade III Higher Division" na "Grade II Local Service Council". Alihamishiwa Mpwapwa mwaka wa 1944 akafanya kazi na Idara ya wanyama hadi 1946. Kutoka 1946 hadi 1952, alifanya kazi ofisi ya mkuu wa Jimbo la Tanga. Kabla ya kustaafu mwaka wa 1959 alifanya kazi na ofisi ya kupima nchi Tanga. Alikuwa mtu mwaminifu, mwenye kupenda urafiki, mvumilivu na mwenye bidii sana. Alipostaafu, akiba ndogo aliyokuwa nayo aliitumbukiza kwa upigishaji chapa uandishi wake. Hii ilikuwa ni kazi ngumu na ya kugharimu fedha nyingi sana. Lakini hakufa moyo kwa maana ilikuwa ni kazi ya hiari na mpenda hiari si mtumwa kama alivyopenda kusema.
Kuanzia mwaka wa 1926 hata1944, Shaaban alifanya kazi na Idara ya Forodha, Pangani. Alikuwa mtu mwenye kufanya kazi yake kwa uangalifu na uvumilivu hata alipandishwa vyeo viwili katika kazi hii: "Grade III Higher Division" na "Grade II Local Service Council". Alihamishiwa Mpwapwa mwaka wa 1944 akafanya kazi na Idara ya wanyama hadi 1946. Kutoka 1946 hadi 1952, alifanya kazi ofisi ya mkuu wa Jimbo la Tanga. Kabla ya kustaafu mwaka wa 1959 alifanya kazi na ofisi ya kupima nchi Tanga. Alikuwa mtu mwaminifu, mwenye kupenda urafiki, mvumilivu na mwenye bidii sana. Alipostaafu, akiba ndogo aliyokuwa nayo aliitumbukiza kwa upigishaji chapa uandishi wake. Hii ilikuwa ni kazi ngumu na ya kugharimu fedha nyingi sana. Lakini hakufa moyo kwa maana ilikuwa ni kazi ya hiari na mpenda hiari si mtumwa kama alivyopenda kusema.
Sheik Shaaban alikuwa hodari kwa
kazi yake ya uandishi na uendelezaji wa lugha ya Kiswahili. Uandishi wake
ulikuwa kazi ya hiyari na matokeo ya mazoezi ya ujana wake. Aliandika hadithi
za mawazo yake kama Kusadikika na Kufikirika,
Historia kama vile utenzi wa vita vya pili vya dunia, Insha, Magazeti, Tawasifu
na vitabu vya wasifu kwa mjazo na ushairi. Lugha aliyoitumia ilikuwa bara bara
na uandishi wake ulihusu mambo yanayotokana na wahenga. Alitilia maanani
desturi iliyoenea na ile inayoelekea kusahauliwa kwa sababu ilitumiwa na
washairi waliotangulia. Uandishi wake ulikuwa na maneno ya hekima tupu na
mafundisho yanayowafaa wake na waume katika ndoa, wajane, watoto na hata wazee.
Hivyo basi, aliweza kutunzwa kwa zawadi ya waandishi inayoitwa "Margaret
Wrong Memorial prize". Alikuwa mwandishi wa kwanza wa Kiwahili kutuzwa
nishani ya "Member of British Empire, (M.B.E.)" kutoka kwa Malkia wa
Uingereza. Tuzo nyingine aliyopata ilikuwa nafasi ya kwanza kwa kuandika insha
juu ya maisha yake katika shindani lililofanywa Afrika Mashariki. Katika
Shindano lingine la uandishi wa insha juu ya utaifa na uzalendo, insha ya
Shaaban ilipata zawadi ya kwanza. Shindano hili lilitolewa na serekali ya Bara
la Hindi.
Katika uendelezaji wa lugha,
Shaaban alijiunga na vyama kama vile, "East African Swahili Committee,
East African Literature Bureau, Tanganyika Language Board, Tanga Township
Authority". Aliheshimiwa Dar es Salaam akawa mtu wa pili kati ya watu kumi
na mmoja kupewa shahada ya kutoka chuoni. Waziri wa Elimu Dar es Salaam mwaka
wa 1966, alimsifu Shaaban na kusema kuwa jina lake limeota mwamba usiobomoka
mioyoni mwa waafrika wengi wa Afrika Mashariki.
Shaaban alifungua duka lake la
vitabu Julai 1960. Alisaidiwa na rafiki yake Mzungu kupigisha chapa katika
kiwanda kingine Kenya. Biashara hii ilikuwa ngumu kwa maana watu wengi walikuwa
hawajui kusoma na kuandika. Wachache waliojua kusoma na kuandika, hawakuwa na
fahamu kwamba katika vitabu ndimo ghala za utamaduni na elimu hupatikana.
Alifurahia kuwapa hawa watu wachache vitabu vyake wasome bure. Hodari huyu wa
lugha ya Kiswahili ameandika zaidi ya vitabu ishirini vya Mashairi. Katika
vitabu vyake, amewashawishi wasomaji wasome mara kwa mara kuendeleza lugha.
Ingawa hayuko sifa zake bado zaenea na vitabu vyake vyatumika kwa ufundishaji
wa lugha katika vyuo vya Tanzania, Kenya na kwingineko ulimwenguni
wanakofundisha lugha ya Kiswahili.
Alifariki tarehe 22
Juni mwaka 1962. Mpaka anafariki kwa maradhi ya moyo na upungufu wa damu, Shaaban
Robert alifanikiwa kuandika vitabu 24 kwa lugha adhimu ya Kiswahili, na mpaka
sasa kazi zake zinazidi kukusanywa na taasisi ya uchunguzi na kukuza
Kiswahili (TUKI) ya chuo kikuu cha Dar es Salaam. Kipo kitabu cha 25 ambacho
kilitolewa miaka ya karibuni ambacho kina barua alizokuwa akiandikiana na jamaa
zake.
Katika kitabu hicho kumeonekana uwezo mkubwa
aliokuwa nao Shaaban Robert katika kuchagua maneno na ufasaha wa lugha ya
Kiswahili na Kiingereza. Kwani watu wengi walidhani Shaaban Robert hakuwa mjuzi
wa lugha ya Kiingereza lakini katika barua zake zipo ambazo aliziandika kwa
lugha hiyo ya kigeni kwa ufasaha wa hali ya juu.
1.3 Muhtasari wa kitabu
Adili na Nduguze ni riwaya iliyotungwa na Shaaban Robert;
mwandishi mashuhuri (maarufu) kutoka Tanzania. Riwaya hii ilitungwa mnamo 1952.
Katika riwaya yake anashughulika na mambo mengi kuhusu tabia mbalimbali za
watu. Mtunzi anatueleza kuwa tushinde uovu kwa kutenda mema yaani “Wema
hauozi”. Adili alimwokoa Huria wakati alipokaribia kuuwawa na Hunde. Kutokana
na wema huo, Huria naye alimwokoa Adili wakati alipotoswa baharini na ndugu
zake. Haya yanazingatiwa na msemo wa Kiswahili “kinifaa huangua, nitakufaa kwa
mvua” au methali isemayo “Mwosha huoshwa”. Katika kufikisha ujumbe mwandishi
ameijenga kazi yake kwa kuwahusisha wahusika mbalimbali. Amemchora Mfalme Rai
kuwa ni kiongozi mzuri na mfuatilizi bora wa kazi ambayo humwezesha kuistawisha
nchi yake ya Ughaibu katika mifugo. Mshauri wake Ikibali alikuwa bingwa wa
uchunguzi wa kodi za wanyama ila alielemewa na siri ya kiongozi wa Janibu,
Adili kuwaadhibu vikali manyani waliokuwa kwake. Alishangaa kuona jinsi ukatili
huo ulivyohitilafiana sana na tabia ya wema na huruma ya Adili akaamua siri
hiyo ifichuliwe mbele ya Mfalme Rai. Alipoletwa mbele ya Mfalme Rai, Adili
alijitetea akieleza kuwa wanyama hao walikuwa zamani nduguze kwani walizaliwa
na baba mmoja, Faraja. Alijulisha kuwa alilazimika kuwagawia urithi wake wakati
walipofilisika ugenini na kurejea nyumbani kwao Janibu. Alisimulia jinsi ndugu
wote watatu walivutwa na faida za biashara na kusafiri mpaka walipoufikia mji
wa mawe, Adili alipokutana na mchumba, Mwelekevu. Hapo hapo, Adili alieleza
kuwa uovu waliomfanyia nduguze ndio uliwafanya wageuzwe kuwa manyani. Kwanza
kutokana na mali aliyoleta jahazini na mwanamke huyo mrembo kutoka mji wa mawe,
nduguze walimwonea wivu na kumlia njama za kumtosa baharini. Wakati huo huo,
aliokolewa na jini, Huria binti Kisasi, ambaye aliwahi kulisaidia
liliposhambuliwa na nyoka, ama jini jingine Hunde. Adili aliporejea katika
chombo akiwa na Huria, jini hilo ndipo liliamua kuwafanya manyani ikiwa ni
adhabu na kutoa amri ya kuwa watapigwa kila siku kutokana na maovu yao. Adili
aliporudi nchini mwake, Ughaibu, ndiye aliadhibiwa wa kwanza kwa kusahau
kuwapiga manyani. Tokea hapo ilikuwa mazoea yake kuwapa chakula na kuwapiga
vikali hadi siku Ikibali alipogundua siri hiyo. Baada ya kisa hicho, Mfalme Rai
almsihi Adili asiwapige tena manyani ila awatunze vizuri na kula nao.
Alijitahidi kuwaombea msamaha kwa Mfalme wa majini Kisasi na bibiye Huria. Ombi
lake lilisikilizwa na nduguze Adili waligeuzwa kutoka uhawayani na kuwa watu
tena. Siku hiyo ilikuwa ya furaha, na nduguze wote watatu walifunga ndoa pamoja.
1.4 Nadharia / mkabala wa Ki-akisiko/kifumano
Nadharia
hii inaelezea fasihi kama inayoakisi uhalisia uliopo nje yake. Mawazo ya aina
hii yanahusishwa na Lenin. Mtaalamu huyu aliziona kazi za Leo Tolstoy kama
zilizoakisi mikinzano ya kijamii iliyoishia kuyasababisha mapinduzi ya Urusi.
Kwa njia hiyo ni kazi za kifanisi. Mkabala huu unategemezwa kwenye itikadi ya
kiujumi iliyokuzwa na Myunani Aristotle katika dhana yake ya ‘muhakati’ au
‘mimesia’ pamoja na msimamo wa Marx kuwa uhalisia ulio wazi au dhahiri
unachukua nafasi ya kwanza kabla ya mawazo akilini. Mhakiki wa Ki-hungary,
George Lukacs anayehusishwa na mkabala huu anaichukulia fasihi kama maarifa ya
uhalisi. Hii haina maana kuwa lazima pawepo na mfanano wa moja kwa moja na
uhalisi. Uhalisi huo lazima ushughulikiwe na ubunifu wa mwandishi, na kazi yake
inayoupa muundo maalum. Katika msingi huu panakuwapo na jinsi mbalimbali za
kuwasilisha uhalisi fulani. Njia hizi hutofautiana katika mkazo wa masuala
fulani yanayoshughulikiwa. Mkabala huu unakuwa msingi mzuri wa kuzitathimini
kazi fulani katika msingi wa uhalisia au utohalisia (Wamitila 2002).
Hivyo
basi, nadharia ya ki-akisiko/kifumano ni nadharia ambayo hujikita katika mambo
yaliyopo yaani uhalisia wenye matukio mahususi na matokeo yanayoweza kuthibitika
na mambo yasiyokuwepo yaani utohalisia ambao matukio yake ni vigumu
kuyathibitisha kama sehemu ya uhalisia. Tukirejelea katika riwaya ya “Adili na Nduguze” mwandishi amejikita
katika uhalisia na utohalisia kwani amezungumzia mambo ambayo yanajitokeza na
yapo katika jamii na yale ambayo ni sehemu ya utohalisia kwani yanasikika
yakisemwa lakini kuyathibitisha kama sehemu ya uhalisia ni vigumu. Hivyo
tutatumia nadharia hii kuhakiki maudhui yaliyojitokeza katika kitabu hiki kwa
kuwa kitabu hiki kinasawiri mambo ambayo yapo katika jamii zetu na yale ambayo
ni utohalisia.
1.5 Nadharia ya Umuundo
TUKI (2004) wanaeleza nadharia kuwa ni mawazo,
maelezo na muongozo uliopangwa ili kusaidia kueleza kutatua au kutekeleza jambo
fulani. Nadharia yoyote ile ya kihakiki ni nyenzo ya kusaidia kufikisha lengo
fulani.
Ntarangwi (2004) anasema kuwa
umuundo waweza kuelezwa kama mtizamo wa kitathimini ambao huzingatia zaidi
miundo inayojenga kazi binafsi. Mwasisi anayetajwa sana katika nadharia
hii ni Ferdinard De saussure aliyependekeza mtizamo mpya kuhusu lugha. Kinyume
na wataalamu wengine walioshughulikia historia na sura maalum za lugha fulani,
Saussure alivutiwa na miundo inayohimili lugha zote, huku akijaribu
kuonyesha kwamba lugha zote za ulimwengu zaweza kutathiminiwa kwa kaida maalum
za umuundo. Alizua istilahi `parole' na `langue' kueleza maoni yake: `Parole'
au uzungumzi ni lugha katika matumizi na hiki ndicho
walichokizingatia wanaisimu wa awali, lakini Saussure alivutiwa na mfumo wa
kinadharia unaounda lugha zote au `Langue' - yaani masharti au kaida
zinazoiwezesha lugha kuwepo na kuweza kufanya kazi. Hata hivyo, kazi ya
Saussure ilikuwa imetengewa wanaisimu peke yao. Katika miaka ya 1950, mtizamo
huo wa Saussure ulianza kusambaa katika masomo mengine hasa wakati mawazo yake
yalipozingatiwa na Mwanaanthropolojia Claude Levi-strauss. Kwa kuchukua maoni
ya isimu ya Saussure na kuyaingiza katika sayansi ya kijamii. Hasa alichotaka
kuendeleza kidhana ni kwamba pana viwango viwili katika kuelewa maisha ya jamii,
isimu, lugha na chochote kingine kile. Viwango hivi ni cha juu juu (surface) na
cha ndani (deep).
Mkondo huu wa mawazo ya umuundo
kuhusu sayansi za jamii ulianzia ulaya na kuathiri mtazamo wa elimu mbalimbali
(duniani) kama vile: Falsafa, Anthropolojia, Historia, Uhakiki wa kifasihi na
Sosiolojia. Kwa hivyo twaweza kuangalia jamii katika muundo wake wa kijuu
juu na kuielewa lakini tukitaka kupata maana mwafaka lazima tuchunguze muundo
wake wa ndani ambao hupatikana katika kila jamii ya wanadamu. Kwa hiyo hata
katika kuielewa fasihi lazima tuifahamu lugha yake. Katika kupata maana
lazima kuwe na uhusiano wa kipembetatu yaani kuna dhana, alama na kitajwa.
Kama vile muundo wa lugha ulivyo
mfumo, muundo wa fasihi pia una vipengele vinavyotegemeana na vinavyoelezwa
katika muktadha wa vipengele vingine. Katika kazi ya fasihi kuna kitengo cha
kisanaa kama vile maudhui, ploti, wahusika, muktadha na lugha. Hakuna kipengele
cha fasihi kati ya hivi kitakachoelezwa katika upekee wake. Lazima kielezwe kwa
kuzingatia kuwepo kwa jukumu la vipengele vingine. Kwa mfano katika kueleza au
kuzungumzia ploti, wahusika watashirikishwa na lugha yao kuzingatiwa. Kwa
hiyo nadharia ya umuundo husisitiza vipengele vya kazi ya sanaa jinsi
vinavyohusiana hadi kuikamilisha kazi hiyo. Huangalia namna sehemu mbalimbali
za kazi za sanaa zilivyofungamana. Yaani Neno halihitaji urejelezi ili lipate
maana, na kazi yenyewe ilivyoundwa ndivyo hutoa maana. Yaani maana inavyoumbwa
ina dhima kubwa kuliko maana yenyewe.
Hivyo nadharia hii tutaitumia katika
kuchambua sehemu ya fani katika riwaya ya “Adili
na Nduguze” kwani nadharia hii itatusaidia kuibua vipengele vilivyoijenga
fani na kuifungamanisha katika kutoa kusudio la Msanii kwa jmii husika.
2.0 Maudhui katika Riwaya ya “Adili na Nduguze”
Kwa
mujibu wa Madumulla (katajwa) maudhui
ni mawazo fikra na ujumbe uliomo katika kazi ya fasihi. Maudhui ina vipengele
mbalimbali ambavyo ni pamoja na dhamira, ujumbe, falsafa, migogoro, msimamo na
mtazamo wa mwandishi. Katika riwaya ya “Adili
na Nduguze” vipengele vya maudhui vinavyojipambanua au kujidhihirisha ni
pamoja na:-
2.1 Dhamira
Madumulla
(katajwa) anasema dhamira ni wazo kuu
katika kazi ya fasihi. Dhamira ni sehemu tu ya maudhui. Dhamira ndiyo hujenga
kiini cha kazi ya fasihi, yafuatayo ni mawazo au dhamira zilizojitokeza katika
riwaya hii ya “Adili na Nduguze”
2.1.1 Uongozi mzuri.
Uongozi ni dhana, taaluma inayompa muhusika
madaraka na uwezo wa kuwawezesha wale wanaoongozwa naye kuunganisha nguvu,
stadi na vipaji vyao na kuvitumia ili kufikia malengo yao. Kuongoza ni kujua
lengo la wale wanaoongozwa na njia ya kufikia lengo lao (www. Sw.wikipedia.
org/wiki/uongozi)
Katika
riwaya hii ya Adili na Nduguze suala la uongozi mzuri limejitokeza. Tunamwona
jinsi Rai alivyokuwa kiongozi muadilifu na mfalme mwema sana katika jamii yake.
Hakuwa na tabia ya kumlazimisha mtu kufanya kazi bali aliwashawishi watu
kufanya kazi. Alijituma katika kufanya kazi kwa bidii zake zote, hakusita
kufanya kazi iwe kubwa au ndogo. Mwandishi anasema;
“Kwa
bidii zake kubwa aliweza kushiriki katika mambo mengi ya maisha, akasaidia
maendeleo makubwa ya nchi yake. Hakulazimisha mtu yeyote kutenda tendo Fulani,
lakini alishawishi kila moyo wa mtu kuiga alivyotenda kwa hiyari yake mwenyewe,
alikuwa na mvuto mkubwa juu ya mioyo ya watu. Alitumia mvuto huu juu ya watu
mpaka nchi yake ilikuwa haina mvivu, goigoi wala mwoga” (uk 2).
Tukilejea
katika jamii ya sasa suala la uongozi mzuri linasisitizwa ili kufikia malengo
ya kimaendeleo. Wapo viongozi ambao ni wazuri na uongozi wao ni bora wakiwa
wanawajibika katika kuangalia maendeleo ya jamii zao.
2.1.2 Matabaka
Kwa
mujibu wa
Katika
riwaya hiii ya Adili na Nduguze suala la matabaka limejitokeza kwani tunaona
kuna matabaka kati ya mtawala na mtawaliwa. Kwa mfano kuna Rai ambaye ndiyo
mfalme wa Ughaibuni na Watawaliwa ambao ndio raia wa ughaibuni. Mwandishi
anasema;
Rai, mfalme wa Ughaibu, alikuwa
mfalme wa namna ya peke yake duniani.
“……Kutawala suluhu na mapenzi ya
wanadamu, utunzaji wa wanyama, na utii juu ya viumbe wasioonekana kama majini
hutaka uwezo mkubwa sana. Kmama hivi, fikiri wewe mwenyewe jinsi Rai
alivyojipambanua mwenyewe na wafalme wengine”.
Tukilejea
katika jamii zetu pia suala la matabaka halipingiki kutokana na kuwepo kwa
mgawanyo wa kazi. Yapo matabaka katika nyanja za uongozi, elimu, siasa na hata
nyanja za kiuchumi na kidini.
2.1.3 Mapenzi ya kweli
Katika
riwaya hii suala la mapenzi ya kweli limejidhihirisha kwani tunamwona muhusika
Adili jinsi alivyokuwa na mapenzi ya kweli na ndugu zake. Kwani hakuwa mbinafsi
kwa kuwa alikuwa tayari kugawana na yeyote chochote alichokuwa nacho. Mwandishi
anasema;
Adili
alikuwa tayari siku zote kugawana na mtu yeyote tonge moja la chakula
lililokuwa mikononi mwake” (uk. 12).
2.1.4 Ukaidi na Dharau
Katika
riwaya hii ya “Adili na Nduguze”
watawala wa mji wa mawe ambao ni mfalme Tukufu na Malkia Enzi na raia wao
walikuwa waabudu mizimu. Walionywa kuachana na tabia hiyo na Mrefu ambaye
alikuwa ametumwa kuja kuwaonya juu ya kuabudu mizimu ambayo ilikuwa ni miti na
matokeo ya kaidi hiyo, mji na watu wote waligeuzwa mawe isipokuwa Mwelekevu
ambaye alikuwa Binti mfalme kutokana na utii wake kiimani. Mwandishi anasema
“Tukufu
hakujali onyo hili akahamrisha kushikwa kwa Mrefu aliyekuwa hasogeleki wala
hashikiki……………, kwa laana iliyotamkwa na Mrefu……………kila kiumbe kilichokuwa na
maisha katika
fahari
kiligeuka jiwe” (uk 29)
2.1.5. Suala la Imani
Imani
lina maana mbalimbali (mfano. "huruma"), na maa kuu inahusiana na
kitenzi kuamini, kinachofanana
na kusadiki. Hapo ni kukubali ukweli
wa jambo lisiloweza kuthibitishwa. Katika dini
msingi wake ni mamlaka
ya Mungu
aliyeshirikishwa ukweli huo kwa njia ya ufunuo
maalumu ili kumsaidia binadamu
amjue yeye, ajifahamu pamoja na maisha yake duniani
na ahera.
Kwa msingi huo, au wa namna hiyo, mtu anaweza kushikilia jambo bila ya
uthibitisho mwingine, ingawa pengine Ukristo
unatia maanani pia akili
katika ujuzi wa ukweli.
Katika
riwaya hii ya ‘Adili na Nduguze’ suala
la Imani limejitokeza kwani tunaona kuwa mfalme Tukufu na malkia Enzi na raia
ambao waliishi katika mji wa Mawe walikuwa wanaamini katika mizimu, Mizimu hiyo
ilikuwa ni miti ambapo baadae miti hiyo iligeuka na kuwa mawe ukutani.
Mwandishi anasema;
“Walakini, juu ya sifa hizo,
malkia, mfalme na raia walikuwa waabudu mizimu. Mizimu yao ilikuwa miti. Miti
yenyewe ni ile iliyogeuka kuwa mawe ukutani. Kawere, mganga na imamu wa mizimu
hiyo alivuta mioyo ya watu wote”(uk. 27).
2.1.6 Suala la ukatili
Suala
la ukatili limejidhihirisha wazi katika riwaya hii. Tunaona jinsi Ndugu zake
Adili (waliitwa Mwivu na Hasidi) walivyomtosa Adili baharini wakati wakiwa
katika jahazi kuelekea Janibu, huku lengo lao likiwa ni kumuuwa ndugu yao ili waweze kumuoa kiushirika Mwelekevu ambaye
alikuwa ni mchumba wake Adili, kutokana na uzuri aliokuwa nao yule msichana.
Mwandishi anasema;
“Alitoswa baharini kama kitu
kilichokuwa hakifai.”
Vilevile
katika jamii zetu suala la ukatili lipo. Kuna watu ambao wamejeruhiwa na hata
kuuawa na ndugu au rafiki zao kwa sababu ya migogoro inayosababishwa na
mapenzi.
2.2 Migogoro
Kwa
mujibu wa TUKI (2004) wanasema kuwa migogoro ni hali ya kutofautiana baina ya
pande mbili au zaidi, wanasema migogoro inaweza kuwa ya familia, matabaka ya
kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. Katika riwaya hii imejitokeza migogoro
tofautitofauti kama ifuatavyo:
Mgogoro
kati ya Mrefu na Tukufu. Mgogoro huu ulitokea baada ya Mrefu kumshauri Tukufu
kuachana na kuabudu mizimu, lakini Tukufu alikaidi. Suluhisho la mgogoro huu ni
kuwa mtu akikaidi mambo ya kiimani hudhurika.
Mgogoro
kati ya Adili na Ndugu zake. Mgogoro huu unatokea pale ambapo Adili aligawa
sawia mali zake kwa nahodha,na ndugu
zake alizozipata kutoka katika mji wa mawe, lakini ndugu zake hawakuridhika
kwani walitaka wapate zaidi. Vivyo hivyo, mgogoro unajitokeza pale ambapo
walimtosa Adili baharini kwa lengo la kutaka kumuoa mchumba wake (Mwelekevu).
Suluhisho la mgogoro huu ni kuadhibiwa kisheria, kutokana na kufanya matendo ya
kihalifu na unyama kwa binadamu.
Mgogoro
kati ya Hunde na Huria. Mgogoro huu unajitokeza pale ambapo Hunde ambaye ni
jini, anamwitaji Huria kimapenzi, ambaye ni mtoto wa mfalme wa majini lakini
Huria anamkataa Hunde. Suluhisho la mgogoro huu ni kuwa Hunde anaemlazimisa
Huria kumkubali kimapenzi ni kushtakiwa kisheria na sheria kuchukuwa mkondo
wake.
2.3 Ujumbe
Kwa
mujibu wa Madumulla (katajwa) ujumbe
ni kitu ambacho mwandishi hudhamiria kumtumia msomaji, kila kazi ya fasihi
hubeba ujumbe ambao msanii hutaka umfikie msomaji wake. Katika riwaya ya hii
kuna ujumbe wa aina tofauti tofauti uliojitokeza kama ifuatavyo:
·
Uongozi mzuri na uadilifu ndiyo chanzo
cha maendeleo.
·
Majuto ni mjukuu
·
Ukaidi na dharau ni chanzo cha madhara
·
Bidii katika kazi ni chanzo cha
maendeleo
·
Imani ni ukombozi
2.4 Falsafa
Kwa mujibu wa Madumulla (katajwa) akimrejelea Msokile (2009) falsafa ni wazo ambalo mtu
anaamini kuna ukweli fulani unaohusu maisha yake pamoja na maisha ya jamii.
Katika riwaya hii ya ‘Adili na Nduguze’ mwandishi
anaamini kuwa uadilifu katika uongozi ni nguzo ya maendeleo katika jamii.
2.5 Msimamo
Kwa mujibu wa Madumulla (katajwa) ni mawazo, mafunzo na falsafa ya msanii. Hubainisha
msimamo wake kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii na ndiyo huweza
kuwatofautisha wasanii wawili au zaidi wanaoandika kuhusu mazingira
yanayofanana. Msimamo wa riwaya ya Adili na Nduguze ni wa kiimani kwani
amesisitiza kuachana na masuala maovu yasiyompendeza Mungu ikiwa ni pamoja na
kuabudu mizimu na badala yake kutenda yale yanayompendeza Mungu na binadamu
ikiwa ni pamoja na kumwabudu Mungu.
Fani katika riwaya ya “Adili na Nduguze”
Fani
ni jumla ya mbinu, ufundi na mtindo wa vipengele vingine vinavyotumika
kuwasilisha maudhui (Mhilu na wenzake 2008). Huu ni ufundi wa kisanaa autumiao
msanii katika kutoa ujumbe wake kwa hadhira iliyokusudiwa. Fani imegawanyika
katika vipengele vikuu viwili ambavyo ni muundo na mtindo
3.1. Mtindo
Kwa
mujibu wa Senkoro (1982) anasema mtindo katika kazi ya fasihi ni ile namna
ambayo msanii hutunga kazi hiyo na kuipa sura ambayo kifani na kimaudhui
huainisha kanuni au kawaida zilizofuatwa (za kimapokeo ama za pekee). Pia
Wamitila (2003) anasema mtindo ni jumla ya mbinu au sifa zinazomwezesha
mwandishi kuwasilisha ujumbe wake, huelezea mwandishi alivyounda kazi yake.
Hivyo
tunaweza kusema mtindo ni ule upekee alionao mtunzi wa kazi ya fasihi katika
kuipa kazi yake sura fulani kifani na kimaudhui ambao mtunzi mwingine hawezi
kufanya hivyo hata kama kinachozungumziwa ni kilekile. Mtindo ndiyo jinsi
msanii alivyotumia ufundi, umahiri na hisia zake katika kutenda au kueleza
jambo fulani. Mtindo huu ndio hutofautisha kati ya msanii mmoja na mwingine.
Katika
riwaya hii ya ‘Adili na Nduguze’ msanii
ametumia mtindo wa masimulizi katika kueleza visa na matukio, kwani tunaona
msanii anaeleza kisa kinachomhusu Adili na nduguze,
Hasidi na Mwivu. Mwandishi anaeleza jinsi vituko vilivyotiririka tokea mwanzo,
ndugu hawa watatu waliokuwa wakitoka familia moja, ndugu wawili, (waovu) Hasidi
na Mwivu, waliomfanyia Adili na malipo ya uovu huo (kama upeo wa kugeuzwa
manyani na kupata adhabu ya kupigwa kila siku). Mwishoni kabisa anaujadili
msamaha waliopewa ndugu hao. Kutokana na majuto na ahadi ya kutorudia tena uovu
huo.
Pia msanii ametumia mtindo wa nyimbo ili kufikisha ujumbe. Mfano
katika uk. 26, msanii ametumia nyimbo katika kutoa sifa ya msichana mrembo
aliyekutana na Adili katika mji wa mawe. Vilevile katika uk. 42, msanii
ametumia nyimbo akionyesha jinsi Adili alivyokuwa akijutia kuwaadhibu ndugu wa
damu yake. Pia msanii ametumia nyimbo katika uk. 48 ambapo uliwakilisha
kusherekea baada ya kupata msamaha kutoka kwa mfalme wa majini.
Aidha,
msanii ametumia mtindo wa barua katika uk. 44, ambapo amemchora mfalme Rai
akiandika barua kwa mfalme wa majini inayohusu kuomba msamaha kwa ajili ya
ndugu zake Adili waliogeuzwa manyani kusamehewa. Na matokeo yake msamaha
wanaupata na kurudi katika hali yao ya kawaida.
3.2 Muundo
.
Hapa tunachunguza jinsi msanii wa kazi ya fasihi anavyofuma, unda na
kuunganisha matukio moja baada ya jingine, wazo na wazo, ubeti na ubeti, hata
mstari wa ubeti. Baadhi ya vipengele vya kimuundo vinavyotumika zaidi ni
mistari, beti, mizani na vina. Hivyo, katika muundo tunaangalia umbo la kazi ya
fasihi mfano, yaweza kugawanywa katika sura mbalimbali, sura hizi ndizo hujenga
muundo
Mtindo wa riwaya hii ni mtindo wa rejea. Mwandishi huanza kuisimulia
riwaya yake wakati Adili anapofanya ukatili wa kuwaadhibu manyani (ambao
walikuwa nduguze). Kugundulika kwa uovu huu ndiko kulifuatiliwa na maelezo ya
kisa na sababu ya nduguze kuwa manyani na hatimaye kuwa watu tena baada ya ombi
la Mfalme Rai kukubaliwa na majini.
Muktadha
Muktadha
ni jumla ya mazingira ambamo kazi ya fasihi inafanyikia. Muktadha wa riwaya hii ni ya nchi ya Ughaibu, yaani nchi ya
mbali. Nchi hiyo ni ya kufikirika kwa kuwa haipo katika mazingira ya kawaida.
Kuna vituko vichache vilivyotokea katika nchi za kigeni zisizotajwa kwa majina
na vingine vilitokea katika nchi ya majini.
3.5. Wahusika
Wahusika
katika riwaya ya “Adili na Nduguze”,
wana majina yanayowiana na tabia zao. Wale ambao hawakubadilika kitabia kama
Adili, Mfalme Rai ni wahusika bapa. Wahusika Huria, Hasidi na Mwivu ambao
walibadilika kitabia ni wahusika duara. Wahusika hao na sifa zao ni kama
ifuatavyo:
3.5.1 Adili
Huyu
ni mhusika mkuu wa riwaya hii. Alikuwa mwema, mwenye huruma, msamehevu,
mvumilivu na mwenye mapenzi ya kweli, jasiri na mfanyabiashara hodari. Tabia
yake ile haikubadilika toka mwanzo hadi mwisho wa hadithi. Kwa hiyo, tabia yake
ni mhusika bapa kielelezo.
3.5.2 Hasidi na Mwivu
Hawa
ni ndugu zake Adili. Walikuwa watu wakatili, wenye tamaa, choyo kubwa na wabadhilifu
kitabia, kwa hiyo ni wahusika duara.
3.5.3
Mfalme Rai
Huyu
alikuwa mtawala wa nchi ya Ughaibu ambaye aliiletea nchi yake ustawi wa
kiuchumi kutokana na uongozi mzuri, ufuatilizi bora wa kazi na ushauri wa
kuwahimiza raia kuwa wachapakazi.
3.5.4 Ikibali
Huyu
ni mshauri wa Mfalme Rai na halmashauri yake. Alikuwa mcheshi na mtu
aliyechukuana na watu kutokana na kuwatunzia haki zao.
3.5.5 Mwelekevu
Huyu ni msichana mwenye upendo wa kweli,
mrembo na mwaminifu kidini na kindoa.
3.5.6 Huria
Huyu
ni jini aliyekuwa na uwezo mkubwa wa kutenda kila jambo alilotaka na kujigeuza
sura kwa utashi wake (mhusika duara)
3.5.7 Mfalme Tukufu na Malkia Enzi
Hawa
ni watawala ambao walipuuzi/walidharau ujumbe wa Mola, wakaadhibiwa kugeuzwa
mawe, mji wao na raia wao.
3.5.8 Mfalme Kisasi
Huyu
ni mfalme wa majini aliyewaelekeza raia wake majini kutii uongozi wa binadamu.
3.3 Matumizi ya lugha
Williady
(2015) anaeleza kuwa matumizi ya lugha ni ustadi wa msanii katika kutumia lugha
itakayoleta mvuto kwa wasomaji au wasikilizaji wa kazi ya fasihi.
Lugha ya Shaaban Robert katika riwaya ya Adili na nduguze ni
rahisi na inayoeleweka. Ni lugha yenye msamiati wa kawaida, misemo ya kawaida,
nahau na methali nyingi. Pia ametumia lugha ya ushairi, lugha ya picha na
tamathali za usemi za kipekee. Kuna wakati mwandishi huyu alipotumia lugha ya
kisheria katika barua, na hayo yote ni kuonyesha jinsi ana ustadi wa kuimudu
lugha ya Kiswahili katika nyanja zake zote.
3.3.1 b) Matumizi ya
methali, nahau, mashairi na misemo
2.2.1.1
Misemo
Misemo
ni maneno yanayotumiwa na makundi maalumu ya watu katika jamaii yaliyo jitenga
kwa kufuatana na mambo yanayo pendelea, mazoea, kazi au shughuli yao, nafasi
yao katika jamii. Ni semi fupi amabazo hutumiwa mara kwa mara kwa lengo la
kuleta maana maalumu. (Mwansoko 1994) Misemo iliyotumika katika riwaya ya Adili
na Nduguze ni;
(i)
Atakaye makaa ya mgomba hapati kitu ila jivu tupu (uk. 39.)
(ii)
Damu nzito kuliko maji (uk. 40)
(iii)
Mwenye saburi hukidhiwa haja zake (uk. 45)
(iv)
Busara kubwa kichwani haina faida kama moyoni hamna chembe ya wema
(uk. 10).
i)
Methali
Ni usemi
mfupi w matokeo unaodokeza kwa muhtasari fikra au mafunzo mazito yatokanayo na
uzoefu wa maisha ya jamii husika. Kauli fupi zenye pande mbili za fikra(www.
Wikipedia.org)
Methali
zilizojitokeza katika riwaya ya Adili na Nduguze ni;
(i)
Mtu huchuma juani akala kivulini (uk. 14).
(ii)
Mali bila daftari hupotea bila habari (uk. 12).
c) Matumizi ya nyimbo
Katika riwaya ya Adili na Nduguze, mwandishi ametumia nyimbo ili
kuwasilisha ujumbe alioukusudia kwa hadhira. Nyimbo zimetumika katika (uk.26,
42, 48)
Mfano katika uk. 26 mwandishi anasema;
“ Miguu ya msichana,
Na mwendo aliokwenda,
Adili alipoona,
Moyowe ulimshinda.
2. Alikuwa na miguu,
Mfano wa cherahani,
Wala ulimwengu huu,
Hajatokea kifani.
Msanii alitumia ushairi
kueleza kwa usanii uzuri wa Mwelekevu”
Tamthali za usemi
Senkoro
(1984) anasema tamathali za semi ni maneno, nahau au sentensi ambazo hutumiwa
na wasanii ili kutia nguvu katika maana, mtindo na hata sauti katika maandishi
ama kusema. Pia Msokile (1992) anasema tamathali za semi ni fungu la maneno
lilogeuzwa maana yake kamili ili kuiwakilisha maana nyingine.
Hivyo
basi, tamathali za semi ni matumizi ya maneno kwa namna fulani ili kuifanya
lugha iwe ya kuvutia na kuifanya kazi ya sanaa iwe ya kupendeza. Vipengele vya
tamathali za semi ambavyo mwandishi amevitumia katika riwaya ya ‘Adili na Nduguze’ ni pamoja na
tashibiha, sitiari, taswira, tashihisi na tafsida. Vipengele kama hivyo ni
muhimu sana katika kuunda au kutoa msisitizo wa maana pamoja na kuunda maana
mpya katika kazi ya fasihi.
- Tashbiha:
Hii
ni mojawapo ya tamathali za semi ambayo inafanya kazi ya kulinganisha vitu
viwili visivyo na hadhi sawa kwa kutumia viunganishi kama vile mithili ya,
kama. Tamathali hii ya semi huweza kufanya kazi endapo kuna vitu
vinavyolinganishwa wakati kimoja hutumiwa katika kukirejelea kingine. Katika
riwaya hii ya ‘Adili na Nduguze’
tashibiha zilizotumika ni pamoja na;
(i)
Moyo wake ulifumwa na msiba
akalia kama motto mdogo (uk.41).
(ii)
Tabia yake ijigawa katika theluthi tatu
mbalimbali kama rangi ya ngozi ya pundamiliya (uk. 1)
(iii)
Alitoswa baharini kama kitu
kilichokuwa hakifai (uk. 3)
Tashihisi
Mhilu na wenzake (2008) anasema tashihisi ni
tamathali ambayo vitu visivyo na sifa walizonazo watu hupewa sifa hizo. Hivyo, tashihisi ni vitu kama vile jiwe, mti
na hata kichaka hupewa sifa ya kutenda kama binadamu afanyavyo. Katika riwaya
hii, Tashihisi zilizotumika ni pamoja na;
(i)Wakati
umefika wa mawe kusema, miti kujibu na wanyama kuwa watu (uk. 9).
(ii)
Mimea hii ilieneza neema ya vyakula kwa watu na malisho ya wanyama (uk. 3).
(iii)Mazizi
yote katika miliki yake amekwishalipa kodi zake, ila mazizi ya Janibu (uk.3).
(iv)Atasema
kweli, na manyani yatakuwa mashahidi (uk. 9)
Mjalizo
Hii ni aina ya
tamathali za semi ambazo msanii/mwandishi huitumia kutaja vitu au mambo yaliyo
katika orodha bila kutumia viunganishi
(i)
Zilipatikana pacha katika
mbuzi, kondoo, ng’ombe, farasi na wanyama wengine (UK. 1)
(ii)
Sebule hiyo ilikuwa
imesakifiwa kwa marmar za rangi tatu, yaani, nyeupe, nyekundu na samawati (uk.
5).
MAREJEO
Senkoro,
F.E.M.K (1982) Fasihi. Dar es salaam: Press and Publicity Centre.
Wamitila,
K.W. (2003) Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Andishi. Naiobi: Focus Publishers.
26
Mhilu,
G. G na Masebo, J. A (2008) Kiswahili kwa
Shule za Sekondari Kidato cha Tatu. Nyambarinyangwine
Publishers: Dar es salaam.
Mulokozi,
M. M. (1996). Fasili ya Kiswahili.
Chuo kikuu huria cha Tanzania: Dar es Salaam
TUKI
(2004) Kamusi ya Kiswahili Sanifu.
Oxford University Press: Dar es saam.
Maoni
Chapisha Maoni