MUHAMMED SAID ABDULLA
Muhammed Said Abdulla alizaliwa April 25, 1918, Makunduchi, Zanzibar katika familia ya kiisramu. Alipata elimu yake ya sekondari katika shule ya wamisionari (missionary school) na baada ya kuhitimu mwaka 1938 alianza kufanya kazi ya ukaguzi (Inspector) katika idara ya afya (civil health depertment). Baada ya miaka 10 aliamua kuwa mwandishi wa habari, na mhongo mmoja baadae alikuwa mhariri msaidizi wa Al Falaq, Al Mahda, na Afrika Kwetu. Mwaka 1958 alikuwa mhariri wa gazeti lililoitwa mkulima (the national agricultural magazine) ambapo hadi kustaafu kwake alikuwa akifanya kazi ya uhariri wa gazeti hilo mwaka 1968.
Baada ya Abdulla kuwa mhariri katika gazeti la mkulima ndipo mafanikio yake ya mwanzo katika uandishi wa riwaya yalipoonekana baada ya kuandika riwaya ya Mzimu wa Watu wa Kale (“1960 “Shrine of the Ancestors”) na ndiyo kazi nzuri ya Kiswahili ya mwanzo ambayo iliingizwa katika mashindano ya mwaka 1957-58 yaliyofanya na taasisi ya Fasihi ya Africa mashariki na hatimaye kuchapwa kuwa ni Riwaya mwaka 1966. Katika kazi hiyo Abdulla aliwatumia wahusika kama Bwana Msa. Ni hadithi ya upelelezi ambayo mhusika wao mkuu ni Bwana Msa. Abdulla aliwatumia wahusika wengine ambao aliludia kuwatumia katika kazi zingine kama Kisima cha Giningi (1968; “The Well of Giningi”), Duniani Kuna Watu (1973; “In the World There Are People”); Siri ya Sifuri (1974; “The Secret of the Zero”); Mke Mmoja Waume Watatu (1975; “One Wife, Three Husbands”); na Mwana wa Yungi Hulewa (1976; “The Devil’s Child Grows Up”).
Katika kuunda majina mapya ya vitabu vyake alivyokuwa akiendelea kuvitoa matumizi yake ya lugha ya Kiswahili kisanaa yalishika hatamu Afrika mashariki na kazi zake ziliendelea kuludiwa kupigwa chapa mala kwa mala pale ambapo zilianza kutumika kama vitabu vya kiada na ziada katika kufundishia mashuleni. Vitabu hivi vilisaidia kupunguza hali ya ujinga wa watu na kuwafanya wawe wenye kutafta maarifa na kuchunguza mambo.
Abdulla kupitia vitabu vyake aliinyanyua lugha ya kiswahili katika daraja la juu na kuiongezea umaarufu mkubwa eneo la afrika mashariki. Alifanikiwa kuowa mke na kupata watoto wawili katika maisha yake. Vile vile ni miongoni mwa watetezi wakubwa waliofanya utetezi katika kuikomboa nchi ya Zanzibar kutoka mikononi mwa Watanganyika. Na hii ndio ilikuwa sababu ya yeye kuwa katika hatari ya maisha yake. Miongoni mwa beti zake za kuwatupia watanganyika ni ujumbe utakaoweza kuwapotezea nguvu ya kutaka kuinyakuwa Zanzibar. Kutokana na jitihada zake njama ilianza kupangwa na watanganyika ili kumuondoa Bwana Msa Katika hii dunia. Hatimaye mkewe na watoto wake wawili wa kike waliuawa katika kipindi cha mapinduzi ya Zanzibar. Hili lilikuwa pigo kubwa sana kwa Wazanzibari wote kwa kupatwa na majonzi katika familia ya mtetezi wao. Abdulla alifariki machi 1991 akiwa na umri wa miaka 72-73.
Muhammed Said Abdulla Ameandika vitabu nane ambavyo ni kama ifuatavyo;
Mzimu wa Watu wa Kale (1960)
Kisima cha Giningi (1968)
Duniani Kuna Watu (1973)
Siri ya Sifuri (1974)
Mke Mmoja Waume Watatu (1975)
Mwana wa Yungi Hulewa (1976)
Kosa la bwana msa (1984)
Kivuli kinaishi(1980)
SAID AHMED MOHAMED
Said Ahmed Mohammed alizaliwa pemba huko Zanzibar, Mnamo tarehe 12 Desemba 1947. Hakubahatika kupata malezi ya baba na mama ipasavyo kwani wazazi wake walitengana akiwa mdogo sana. Hivyo alilelewa na mama zake wakuu (mama zake wakubwa), Bi. Jokhana Bi Rukia. Alisoma shule ya msingi Wete Boys,Pemba baadaye alihamia Kiembe samaki, Unguja. Kisha akapelekwa skuli ya Darajani (shule yenye watoto wenye vipaji) Unguja baadaye akaendelea na masomo yake ya sekondari katika shule ya upili ya Gulioni ambapo zamani iliitwa “King George The VI”. Mapinduzi ya Zanzibar yalitokea akiwa kidato cha pili. Baada ya kuhitimu masomo yake ya sekondari alijiunga na chuo cha ualimu cha Nkurumah TTC kilichopo mjini Zanzibar mwaka 1966, ilishindikana kujiunga na kidato cha tano na sita kwani wakati huo kiongozi wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar hayati Abeid Aman Karume alipiga marufuku masomo ya kidato cha tano na sita.
Baada ya kuhitimu chuo alifundisha shule ya msingi Kizimbani kwa wiki mbili tu, halafu akahitajika kwenda kufundisha shule ya sekondari Utaani, kuanzia 1969 hadi 1974. Saidi Ahmed Mohamed alifundisha masomo ya biologia, hesabu, kemia na pia Kiswahili. Baadaye alibahatika kusoma katika skuli ya International Correspondence kiwango cha kidato cha tano na sita. Baada ya kujiunga na kidato cha tano na sita alipanga kujifunza masomo ya sayansi lakini palikosekana vifaa vya kufanya masomo ya utekelezaji wa kisayansi yaani (practical) na hivyo alichagua kufanya masomo ya kisanaa.
Mnamo mwaka 1976 Said Ahmed Mohammed alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es salaam kusomea shahada ya kwanza katika elimu akijikita katika kusoma Isimu na Fasihi ya Kiswahili, baada ya kufuzu katika shahada hiyo alirejea nyumbani Zanzibar na kuwa mwalimu mkuu wa shule za msingi na upili za Hamamni kwa miaka mitatu. Na baadaye alirudi Chuo Kikuu cha Dar es salaam na kujisajili kusomea shahada ya uzamili yaani (MA), katika Isimu Telekezi. Alipokuwa akisoma Chuo Kikuu cha Dar es salaam kipawa chake kilimvutia mwalimu kutoka Ujerumani aliyefundisha Isimu Linganishi na ya kihistoria bwana Sigmund Bruner. Hapo ndipo alipopata fursa ya kuelekea Ujerumani kufanya shahada ya uzamifu yaani PhD, alijiunga na Chuo Kikuu cha Karl Marx Leipzig Ujerumani mwisho wa mwaka 1981 na kukamilisha shahada ya uzamifu mwaka 1985 na kutunukiwa shahada ya udaktari, kipindi hicho alikuwa pamoja na familia yake.
Baada ya kumaliza shahada yake ya uzamifu huko Ujerumani aliteuliwa na raisi wa Zanzibar wakati huo mzee Idris Abdul Wakil, kuwa mkurugenzi wa pili wa Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI), ambayo baadaye ilikuwa Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), hivyo kurejea nyumbani Zanzibar kwa miaka miwili na baadaye akaondoka kwa sababu za kisiasa na fitina za watu ambao haku wafahamu, akaelekea Kenya mnamo mwaka 1987 na kuwa mwenyekiti wa kwanza wa idara ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Moi mjini Eldoret na baadaye kufundisha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Nairobi hadi mwaka 1990.
Said Ahmed Mohammed aliondoka Kenya kutokana na matatizo aliyokumbana nayo Moi-Kenya. Tatizo kubwa ni mtoto wake ambaye alifanyiwa visa mbalimbali kama vile kutafunwa meno na mtoto wa kikenya na suluhu ya kisa hicho haikuwa sahihi kwa mujibu wake. Sababu ya kisa hicho ni utundu wa watoto pamoja na kasumba ya utaifa ambayo iliwafanya kumuona ni mgeni na kuanza kumnyanyasa. Hivyo kwa kuwa hakupenda wanawe wateseke aliamua kuacha kazi kwani ilifikia hatua watoto wake hawakutakiwa kupanda gari ya shule. Alipotoka Nairobi alielekea Japan katika Chuo Kikuu cha Osaka, idara ya lugha za kigeni na hapo ndipo alipopata uprofesa. Alipotoka Osaka ndipo akaenda Chuo Kikuu cha Bayreuth, Ujerumani na kufundisha tangia mwaka 1997 mpaka 2012.
Said Ahmed Mohammed alipenda kusoma, kutunga mashairi na hadithi fupi, alipokuwa darasa la tano alitungama mashairi yaliyotumiwa na walimu katika madarasa ya juu. Kazi yake ya mwanzo ni utunzi wa shairi ambalo liliitwa “Nimfuge Ndege Gani Ili Nipate Salama” mwaka 1960. Shairi hili lilifungua mdahalo mkubwa kwa wapenzi wa fasihi na wana fasihi. Baada ya hapo alipata hamu kubwa ya kuendelea kuandika. Hivyo aliandika mashairi na kupeleka redio ya Zanzibar. Alipata hamasa zaidi kutoka kwa walimu wake ambao ni Mohamed Abdallah, na Kindi Abubakary ambao waliona kipaji chake na kumsisitiza aandike.
Said Ahmed Mohammed aliwahi kushiriki mashindano yaliyoanzishwa na idara ya Kiswahili BBC. Mashndano hayo yalihusu uandishi wa hadithi fupi za Kiswahili. Mara nyingi hadithi zake zilishinda, na hadithi ya “Sadiki Ukipenda” ndiyo iliyompa umaarufu, katika hadithi hii mtunzi alionesha umakini wake katika kutunga visa bunilizi ambavyo vilielezea maisha halisi ya kila siku katika jamii.
Said Ahmed Mohammed alirithi kipawa cha usanii kutoka kwa mama yake mkubwa ambaye alikuwa nyakanga. Mama huyu alikuwa bingwa wa kuimba nyimbo za unyago. Pia alikuwa mtunzi mzuri wa mashairi, na alipenda sana hadithi za fasihi simulizi. Uandishi wa Said Ahmed Mohammed zaidi ya kurithi kutoka kwa mama yake mkubwa, ulitokana pia na mafunzo ya elimu ya dini ya kiislam, aliyoipata kutoka madrassa.
Said Ahmed Mohammed alivutika na kuanza kusoma riwaya, riwaya ya mwanzo kuisoma ilikuwa ni riwaya ya Kiu( 1972), ikifuatiwa na Nyota ya Rehemu (1976), zilizotungwa na Mohamed M.S. Baada ya kusoma riwaya ya Kiu ndipo alipopata hamu na shauku ya kuandika riwaya. Riwaya yake ya mwanzo aliyoiandika ni Asali Chungu (1977), ikifuatiwa na Utengano (1980), na Dunia Mti Mkavu (1980). Aliendelea na jitihada za uandishi hadi kuwa muandishi maarufu na kupata tuzo mbalimbali ndani na nje ya nchi. Vilevile amebobea katika ushairi ambapo ametunga diwani mbalimbali, zikiwemo za kisiasa, kiuchumi, mapenzi na utamaduni. Diwani hizo ni kwa lengo la kuibua maudhui aliyokusudia muandishi huyu kama waandishi wengine wa kazi za fasihi. Ametumia fani katika kazi zake za fasihi mojawapo ya mitindo aliyotumia ni uhalisia mazingaombwe katika kazi kama vile, “Babu alipofufuka, Kivuli Kinaishi, Amezidi na Sadiki Ukipenda, pia alitumia bunilizi, utomeleaji na taswira katika kazi zake nyingi.
Said Ahmed Mohammed ametajwa kama muandishi mashuhuri zaidi Africa Mashariki na hata Afrika nzima akiwa ameweza kuandika Riwaya, Tamthilia na Mashairi, kazi za watoto na hata vitabu vya shule na vyuo. Baadhi ya kazi zake zimetafsiriwa kwa lugha za kigeni, pia kuna miswada ambayo imechapishwa hivi karibuni ya riwaya ya Nkama dume, Mhanga Nafsi yangu, na kitabu cha kusoma katika darasa la saba kiitwacho Gharama ya Amani kinachozungumzia fujo za kisiasa zilizotokea Kenya. Mwandishi huyu ni miongoni mwa waandishi wa riwaya za kimapinduzi na kifalsafa.
Profesa Said Ahmed Mohammed ana mke mmoja anayeitwa Rahma, na watoto wawili msichana na mvulana. Msichana anaitwa Najima jina linalo maanisha nyota na wa kiume anaitwa Mahirna neno la kiarabu lenye maana ya mwenye ujuzi na wote wamekamilisha shahada ya kwanza.
Profesa Said Ahmed Mohammed Ameandika zaidi ya vitabu 60, cha karibuni zaidi kikiwa Mashetani Wamerudi, tamthilia iliyozinduliwa rasmi Oktoba 10, 2016 katika Tuzo za Kumi - Kumi ambazo hutolewa kila mwaka na mwasisi wa WASTA Kituo cha Kiswahili Mufti, Guru Ustadh Wallah Bin Wallah.
Baadhi ya vitabu alivyoandika ni kama ifuatavyo:
Ushairi Kama vile:
Sikate Tamaa (1980) Longman Kenya Ltd.
Kina cha Maisha.
Jicho la Ndani (2001), Nairob: Longhorn Publisher.
Tamthiliya;
Pungwa (1988), Longman Kenya Ltd.
Kivuli kinaishi (1990), Oxford University Press.
Amezidi (1995), East African Educational Publishers.
KitumbuakimeingiaMchanga (2004) Nairob: Longhorn Publishers ltd
Posaza Bi Kisiwa
Riwaya;
Asali Chungu( 1989), East Afracan Publishers.
Babu Alipofufuka (2001), JomoKenyatta Foundation.
Utengano (1980), Longhorn Publishers.
Tata za Asumin i(1990), Longman Kenya.
Dunia Mti Mkavu (1980), Longman Kenya Ltd.
Kiza Katika Nuru (1988), Oxford University Press.
Dunia Yao (2006), Nairob:Oxford University Press.
EUPHRASE KEZILAHABI
Euphrase Kezilahabi alizaliwa mwaka 1944 katika kijiji cha Namagondo kilichoko kisiwani Ukerewe katika ziwa Victoria nchini Tanzania. Alisoma shule ya msingi ya Nakasayenge halafu tangu 1957 Seminari ya kikatoliki ya Nyegezi aliyomaliza mwaka 1966. 1967 alijiandiskisha kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akasoma ualimu na fasihi hadi digrii ya B.A. katika mwaka 1970. Mwaka uleule 1970 akawa mwalimu wa shule ya sekondari Mzumbe (Morogoro) halafu kwenye shule ya sekondari ya Mkwawa (Iringa). Katika masomo yake alijishughulisha na nadharia mbalimbali zihusuzo falsafa (Wamitila 1991:64). 1971 alirudi chuoni Dar es Salaam akawa mhadhiri msaidizi wa chuo alipoandika pia tasinifu ya M.A. kuhusu riwaya za Shaaban Robert, tangu 1974 mhadhiri kamili na 1978 mhadhiri mwandamizi. Akaendelea na masomo ya Ph.D. huko Marekani kwenye Chuo Kikuu cha Wisconsin Madison alipotoa tasinifu yake mwaka 1985 kuhusu "African Philosophy and the Problem of Literary Interpretation". Baada ya masomo yake huko Marekani alirudi kufundisha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam kabla ya kuhamia Chuo Kikuu cha Botswana ambako anafundisha Lugha za Kiafrika na Fasihi.
Katika maisha yake Kezilahabi ametunukiwa tuzo kadhaa kutokana na uandishi wake. Miongoni mwa tuzo hizo ni ile ya kumbukumbu ya Edoardo Sanguinetti (1990) na ile ya kumbukumbu ya Shaaban Robert (1995) (Mezger 2002: 76).
Kezilahabi ameandika kazi kadhaa kama vile zifuatazo:
Riwaya:
Rosa Mistika (1971)
Kichwamaji (1974)
Dunia Uwanja wa Fujo (1975)
Gamba la Nyoka (1979)
Nagona (1987/1990)
Mzingile (1991)
Mashairi:
Kichomi (1974)
Karibu Ndani (1988)
Dhifa (hakijatolewa bado)
Tamthiliya:
Kaptula la Marx (1978/1999)
Hadithi fupi:
Mayai Waziri wa Maradhi
Cha Mnyonge Utakitapika Hadharani
MAREJEO
Diegner, L. (2005) Intertextuality in the Contemporary Swahili Novel: Euphrase
Kezilahabi’s Nagona and William E. Mkufya’s Ziraili na Zirani. Kiswahili
Forum 12 (uk. 25-35).
"Euphrase Kezilahabi". www.poetrytranslation.org. Retrieved 2017-03-30
Gromov, M. D. (1998) Nagona and Mzingile: Novel,Tale or Parable? AAP55 (uk.73-78)
Hoiberg, Dale H, ed. (2010) “Abdulla muhammed said” Encyclopædia Britannica
Kezilahabi, E. (1990) Nagona. Dar es salaam, Dar es salaam University Press.
…………… (1991) Mzingile. Dar es salaam, Dar es salaam University Press.
Wamitila, K. W. (1991) Nagona and Mzingile: Kezilahabi’s Metaphysics. Kiswahili:
Jarida la Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili Juz. 58.
………………. (1997) Contemptus Mundi and Carpe Diem Motifs in Kezilahabi’s
Works. Kiswahili: Jarida la Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili Juz. 60.
Zubkova, Elena Bertoncini (2008) “Abdulla muhammed said”Dictionary of African Biography. Oxford University Press.
Maoni
Chapisha Maoni