UCHAMBUZI WA RIWAYA ZA “NAGONA” NA “MZINGILE” 1.0 Utangulizi Katika makala haya tutachambua riwaya za ‘Nagona’ na ‘Mzingile’. Katika kuchambua riwaya hizi tutajikita katika kuangalia baadhi ya vipengele kama dhamira, falsafa, lugha, mtindo wa usimulizi, wahusika, motifu na suala la ontolojia. 2.0 Maelezo kuhusu mwandishi na riwaya zake 2.1 Maelezo kuhusu mwandishi Euphrase Kezilahabi alizaliwa mwaka 1944 katika kijiji cha Namagondo kilichoko kisiwani Ukerewe katika ziwa Victoria nchini Tanzania. Alipata elimu ya msingi huko kijijini Ukerewe na baadaye alijiunga na seminari ndogo ya Nyegezi kwa ajili ya masomo ya upili. Baada ya kumaliza alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es salaam mnamo mwaka 1967. Katika masomo yake alijishughulisha na nadharia mbalimbali zihusuzo falsafa (Wamitila 1991:64). Mnamo mwaka 1976 alitunukiwa shahada ya umahiri ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, kabla ya kutunukiwa shahada nyingine ya umahiri ya Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison mwaka 1982. Mwaka...